1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bilionea la Kijerumani lajiua baada ya biashara zake kwenda mrama

Aboubakary Jumaa Liongo7 Januari 2009

Tajiri mmoja mkubwa hapa Ujerumani aliyekuwa akimiliki makampuni na viwanda kadhaa,Adolf Merckle amejiua baada ya biashara zake kuingia katika hasara kubwa.

https://p.dw.com/p/GTnF
Bilionea Adolf MercklePicha: picture-alliance / dpa

Billionea huyo wa kijerumani aliyekuwa na umri wa miaka 74 aliamua kujitupa kwenye reli na kukanyagwa na treli huko kusini mwa mji wa Ulm.


Kuyumba kwa uchumi wa dunia ndiko kulikochangia kuzoroto kwa biashara za billionea huyo na hivyo hakuona njia nyingine ila kuiaga dunia kuliko kuona akiwa na mzigo wa madeni.


Mkuu wa polisi katika mji huo Ulm, Wolfgang Zier amesema kuwa familia ya billionea huyo wa Kijerumani ilitoa taarifa polisi ya kutorejea kwake nyumbani, ambapo baadaye zilikuja taarifa za kuwepo kwa ajali ya treni iliyomuhusisha.


Amesema kuwa alijirusha wakati treni ilipokuwa ikipita  karibu na mji wa Blaubeuren.


Tajiri huyo ambaye mwaka jana aliwekwa kwenye orodha ya kuwa mtu wa 95 mwenye fedha nyingi zaidi duniani, na watano kwa utajiri hapa Ujerumani, alikuwa na himaya ya biashara iliyoajiri kiasi cha wafanyakazi laki moja ambapo biashara zake zilikuwa na thamani ya mauzo ya euro billioni 30 kwa mwaka.


Anamiliki makampuni kadhaa makubwa hapa Ujerumani kikiwemo kiwanda cha cement  cha Heidelberg pamoja na kampuni la madawa liitwalo Ratiopharm.


Lakini Merckle ambaye alikuwa baba wa watoto wanne, alijikuta himaya yake yake hiyo ya biashara ikiingia hasara ya takriban euro millioni 400 katika hisa zilizoporoka za kampuni ya magari ya Volkswagen.


Kufutia habari za kifo hicho hisa za kampuni hiyo ya cement zilishuka kwa asilimia 12.5 katika soko la hisa la Frankfurt, kwani wengi wa wawekezaji wanahisi kuwa hakutakuwa na mtu atakayeongoza na kusimamia vyema biashara zake.


Waziri wa utafiti wa Ujerumani Annete Schavan ambaye jimbo lake liko katika mji huo wa Ulm alimuelezea Merckle kama mfanyabiashara aliyekuwa na mchango mkubwa kwa jamii.


Naye Waziri Mkuu wa jimbo la  Baden-Wuerttemberg, Guenther Oettinger alimsifu akisema kuwa alikuwa ni mjasiria mali wa kiwango cha juu.


Wakati bilionea hilo la Kijerumani likikatisha maisha yake kwa biashara zake kwenda mrama, nchini Marekani aliyekuwa mkuu wa moja ya makampuni makubwa ya minada ya nyumba amekutwa amekufa kwa kujipiga risasi.


Steve Good alikutwa akiwa ndani ya gari lake kwenye msitu huku mwili wake ukiwa na majeraha ya risasi.


Vifo hivyo pamoja na kile cha  mwezi uliyopita cha tajiri la kifaransa Thierry Magon de la Villehuchet, vimetokana na msukosuko wa uchumi uliyoikumba dunia, ambapo makampuni mengi yameingia katika hasara kubwa.