1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine akosolewa kubadili msimamo mapenzi ya jinsia moja

6 Desemba 2023

Kiongozi wa upinzani Uganda, Robert Kyagulanyi, ameshtumiwa vikali na wanasiasa wa pande zote nchini mwake kwa kuomba msamaha kuhusu msimamo wake wa awali juu ya masuala ya mapenzi ya jinsia moja.

https://p.dw.com/p/4Zqd5
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine).
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine).Picha: Mohammed Khelef/DW

Wiki iliyopita, Bobi Wine alikwenda Uingereza kwa sherehe za uzinduzi wa filamu yake, ikiwa ni baada ya kuwekewa kizuizi cha kuingia nchi hiyo tangu mwaka 2014 kutokana na wimbo wake uliowaponda watu wanaoshiriki  mapenzi ya jinsia moja akitaka wapigwe na wauawe.

Lakini kwenye mahojiano na wanahabari akiwa Uingereza, mwanasiasa huyo  alielezea kuwa amebadilisha msimano wake huo na badala yake akadai kuwa hata  sheria kali iliyopitishwa na serikali Uganda dhidi ya mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja ilikuwa inawalenga wafuasi wake na upinzani kwa jumla.

Soma zaidi: Marekani yawawekea vikwazo vya visa maafisa kadhaa wa Uganda na Zimbabwe

"Nataka nijulikane kama kiongozi anayeheshimu haki za kila mtu. Na hiyo ni mojawapo ya sababu napambana na Jenerali Museveni ambaye alisaini sheria hiyo. Hakuleta sheria hiyo kwa maslahi ya watu wa Uganda lakini aliulenga upinzani, nikiwemo mimi mwenyewe." Alisema mwanasiasa huyo na mwanamuziki maarufu.

Ukosoaji mkali kutoka kwa umma

Baada ya habari hizo kusambazwa kwenye vyombo vya habari, watu mbalimbali wamemkosoa vikali Bobi Wine kwa matamshi yake hayo, huku wenzake kadhaa katika upinzani wakajitenga na tamko hilo.

Bobi Wine (wa pili kushoto) wakati alipohudhuria mkutano wa kimataifa wa vyombo vya habari (GMF) unaondaliwa kila mwaka na DW mwaka 2022.
Bobi Wine (wa pili kushoto) wakati alipohudhuria mkutano wa kimataifa wa vyombo vya habari (GMF) unaondaliwa kila mwaka na DW mwaka 2022.Picha: Björn Kietzmann/DW

Mmoja wao ni mbunge Asuman Basalirwa kutoka chama cha JEEMA, ambaye ndiye aliongoza katika kuandaa muswaada wa sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja. .

Soma zaidi: Polisi Uganda yazuwia mapokezi ya Bobi Wine

Mbunge alisema huenda Bobi Wine ameshazidiwa nguvu na makundi yanayopiga kampeni za mapenzi ya jinsia moja.

"Makundi yanayowapigania mashoga yana nguvu nyingi za ushawishi wa pesa na tunajua baadhi ya wenzetu wamo katika shinikizo na vitisho. Lakini kama taifa tunashikilia msimamo wetu kwamba kama ndoa za mitala ni haramu Ulaya, kwa nini kuwe na shida kuharamisha ushoga Uganda?" Alisema mbunge huyo.

Bunge latowa kauli

Hata spika wa bunge la Uganda alilazimika kutoa tamko rasmi siku Jumatano (Disemba 6), ambapo alisistiza kuwa hatua ya wao kupitisha sheria  hiyo haikutokana na shinikizo la Rais Museveni ila "ni kwa ajili ya kulinda maadili na mustakabali wa raia wa Uganda na Afrika kwa jumla."

"Hatujuti kupitisha sheria hiyo na namshukuru rais wa taifa hili kwa kusaini sheria hiyo. Tutalinda watoto na nchi yetu na hatutategemea kuombaomba kwa sababu tunataka vibali vya kuingia nchi za kigeni." Alisema spika huyo.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda anatuhumiwa na mwanasiasa wa upinzani, Bobi Wine, kupitisha ya kupinga mapenzi ya jinsia moja kuwalenga mahasimu wake wa kisiasa.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda anatuhumiwa na mwanasiasa wa upinzani, Bobi Wine, kupitisha ya kupinga mapenzi ya jinsia moja kuwalenga mahasimu wake wa kisiasa.Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Soma zaidi: Kijana wa miaka 20 ashitakiwa kwa ushoga Uganda

Kulingana na watu mbalimbali, Bobi Wine amejichimbia kaburi lake la kisiasa na hatakuwa na wa kumlaumu kwani amedhihirisha kuwa yuko tayari kupigania haki za jumiya ya wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, bila kujali maslahi ya watu wa Uganda.

Katika taifa hilo la Afrika Mashariki, kama zilivyo nchi nyingine nyingi za Afrika, ushoga unapingwa.

Bobi Wine kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa upinzani baada ya chama chake kukitoa jasho kile chama  kinachotawala cha NRM  katika uchaguzi wa mwaka 2021.