1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit: Kiongozi wa baraza la wawakilishi Uingereza ajiuzulu

Lilian Mtono
23 Mei 2019

Kiongozi wa baraza la wawakilishi, Uingereza Andrea Leadsom amejiuzulu. Leadsom maarufu kwa uungaji mkono Brexit amejiuzulu kutoka kwenye baraza la waziri mkuu Theresa May, kutokana na kukosa imani na mipango ya Brexit.

https://p.dw.com/p/3Ivi9
Großbritannien London Andrea Leadsom bei Erklärung zum Rückzug
Picha: Getty Images/C. Court

Leadsom amesema hana imani tena na njia anayotumia waziri mkuu Theresa May Pendekezo jipya la Waziri Mkuu wa Uingereza kama inaweza kuufanikisha mchakato wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya ama Brexit. 

Leadsom, anayetambulika zaidi kwa uungaji wake mkono Brexit amemuandikia barua waziri mkuu May akimtolea mwito wa kuchukua maamuzi sahihi kwa ajili ya maslahi ya taifa, serikali na chama chao. 

"hakuna aliyetamani ufanikiwe zaidi ya nilivyotamani," aliandika Leadsom, aliyekabana koo na May kwenye kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu Julai 2016, kabla ya kujiondoa. "Ninachokuomba hivi sasa ni kufanya maamuzi sahihi kwa kuangazia maslahi ya taifa, serikali hii na chama chetu," aliongeza Leadsom.

Kujiuzulu kwake kunakuja siku moja kabla ya Uingereza kufanya uchaguzi wa bunge la Ulaya, wakati pia May akikabiliwa na pingamizi kubwa dhidi ya mapendekezo yake ya karibuni katika harakati zake za kuwashawishi wabunge kukubaliana na mpango wake wa Brexit.  

Huku haya yakitokea, May hapo jana aliendelea kupuuza ongezeko la miito ya kumtaka ajiuzulu, licha ya kuongezeka kwa upinzani kutoka kwa wabunge na mawaziri wa chama chake cha Conservative juu ya mpango wake wa karibuni wa Brexit, na hatua ya kujiuzulu kwa Leadsom inazidi kuongeza shinikizo hata zaidi kwa waziri mkuu huyo.

Hata wabunge ambao awali walimuunga mkono May, wamesema hawakubaliani na mapendekezo yake mapya, ambayo miongoni mwake ni kuwataka kuzingatia kura ya pili ya maoni ya Brexit.