1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge lafungwa DRC kutokana na vurugu za kivyama

Daniel Gakuba
8 Desemba 2020

Shughuli za bunge la DRC zimeahirishwa kwa muda usiojulikana, baada ya kikao kukumbwa na ghasia, ambazo wabunge wa muungano wa rais wa zamani Joseph Kabila wanasema zilisababishwa na wenzao wa rais Tshisekedi.

https://p.dw.com/p/3mOGM
Demokratische Republik Kongo Parlament in Kinshasa
Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

"Ndoa ivunjike, ndoa ivunjike"…ndivyo walivyosikika wakiimba wabunge hao wa muungano wa kisiasa wa CACH unaoongozwa na rais Felix Tshisekedi baada ya vurugu kubwa zilizotokea Jumatatu katika chumba cha vikao cha bunge mjini Kinshasa.

Muungano wa kisiasa unaoongozwa na rais mstaafu Joseph Kabila, FCC unawashutumu wabunge wa CACH kuzifanya vurugu hizo, ambamo, kulingana na duru za mwandishi wa habari wa shirika la AFP, meza na viti vilivyokuwa kwenye jukwaa la chumba cha bunge vilisambaratishwa na kuvunjwavunjwa.

Tangazo lililotolewa na ofisi ya spika Jeanine Mabunda, ambaye anatoka upande wa Kabila, limesema vikao vyote vya bunge, vikiwemo vya kamati zake maalumu vimeahirishwa kwa muda usiojulikana. Tangazo hilo limekosoa vikali mienendo ya wabunge wa upande wa Tshisekedi, na pia kuwepo kwa maafisa wa usalama waliojihami kwa silaha katika majengo ya bunge. Kambi ya Kabila inavidhibiti viti zaidi ya 300 katika bungee hilo lenye jumla ya viti 500.

Huku hayo yakiarifiwa, ripoti kutoka Kinshasa zinasema kuwa Jumatatu jioni Rais Tshisekedialifanya mazungumzo na Waziri Mkuu Sylivestre Ilunga ambaye pia ni kutoka upande wa Kabila. Hata hivyo, hakuna maelezo zaidi kuhusu yaliyozungumzwa.

Demokratische Republik Kongo Félix Tshisekedi
Rais Félix Tshisekedi wa DRC katikati na maafisa wa usalamaPicha: Giscard Kusema/Press Office President DRC

Katika tangazo hotuba yake ya Jumapili kwa taifa, Rais Tshisekedi alisema ushirika kati yake na Kabila ambao umekuwa ukiiongoza nchi kwa muda wa miaka miwili iliyopita umevunjika, na kuongeza kuwa ikiwa hataweza kuunda wingi wa kisiasa wa kuweza kuitawala nchi, itabidi kuitishwa kwa uchaguzi mpya.

Tshisekedi aliushutumu muungano wa vyama vinavyoongozwa na mtangulizi wake Joseph Kabila, kukwamisha utekelezwaji wa mageuzi makubwa aliyoyaahidi.

Muungano wa vyama vya upande wa Kabila, FCC ukizungumzia hotuba hiyo ya rais Tshisekedi, umeiita ukiukaji mkubwa wa katiba, na kuwataka wananchi wa Kongo kusimama kidete, dhidi ya kile ulichokitaja kuwa ni jaribio la kushika mateka maamuzi waliyoyafanya kwa uhuru kupitia masanduku ya kura.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeelezea wasiwasi mkubwa kutokana na mvutano huu mpya wa kisiasa katika nchi hiyo yenye historia ndefu ya mizozo, na kuonya kuwa Kongo haiko katika hali ya kuweza kustahimili mgogoro wa kitaasisi.