1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge Sudan kusini larefusha muda wa rais Kiir madarakani

Sekione Kitojo
12 Julai 2018

Bunge la Sudan kusini limepiga kura kurefusha muda wa rais Salva Kiir kubakia madarakani hadi mwaka 2021,amesema spika wa bunge, hatua ambayo inadhoofisha mazungumzo ya amani na makundi ya upinzani.

https://p.dw.com/p/31Lkw
Südsudan Salva Kiir und Paul Malong Awan
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Makundi ya  upinzani  nchini Sudan kusini  katika siku  za  nyuma  yalishutumu  hatua  kama  hiyo  kuwa  inakwenda kinyume  na  sheria. 

Bunge lilipiga  kura  leo kurefusha  muda  wa  kubakia madarakani kwa  rais Salva Kiir kwa  muda  wa  miaka mitatu  zaidi, hatua ambayo bila  shaka  itatatiza juhudi  za  kuleta  amani  katika  nchi hiyo  changa  duniani. Mswada  wa mabadiliko  ya  katiba  katika kipindi  cha  mpito nambari  tano  kwa  mwaka  2018 umepitishwa na bunge  la  taifa," alisema  spika  wa  bunge Anthony Lino Makana baada  ya  wabunge kwa  kauli  moja  kupiga  kura  kupitisha mswada  huo  ambao  si  lazima utiwe  saini  kuwa  sheria  na  Kiir.
 

Südsudan Juba - Riek Machar, Salva Kiir
Riek Machar makamu wa rais wa zamani (kushoto) pamoja na rais Salva Kiir (kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

Sheria  hiyo itamruhusu Kiir kubakia madarakani  hadi  mwaka  2021 hata  wakati  akiwa  anajishughulisha  na  duru  ya  hivi  karibuni kabisa  ya  majadiliano  ya  kimkoa  ya  amani  pamoja  na  makamu wake  wa  zamani  ambaye  hivi  sasa  ni  kiongozi  wa  waasi  Riek Machar katika  kumaliza  vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe  vya miaka  minne  sasa.

Uchaguzi ulikuwa  ufanyike mwaka  huu, lakini  mzozo  umesababisha muda  wa  kufanyika  uchaguzi  huo  kushindikana. Waziri  wa  sheria Paulino Wanawilla , ambaye  aliwasilisha  mswada  huo, alisema utazuwia serikali  kutangazwa  kuwa si  halali, wakati  muda  wake wa  kuwapo  madarakani  utakapomalizika.

Kiir  na  Machar waliingia  vitani Desemba 2013.

Tangu  wakati  huo mamia kwa  maelfu  ya  watu  wameuwawa  na mamilioni  wengine wamelazimika  kukia  makaazi  yao, na  kuzusha mzozo  mkubwa  wa  wakimbizi  katika  kanda  hiyo pamoja  na kiasi kikubwa  cha  njaa.
 

Südsudan | Unterzeichnung Waffenstillstandsvereinbarung
wakishikana mikono baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano,Kuanzia kushoto kwenda kulia , rais Salva Kiir, Omar al-Bashir rais wa sudan na Riek MacharPicha: REUTERS

Mazungumzo ya amani 

Duru  kadhaa  za  mazungumzo, yaliyosimamiwa  na  kundi  la mataifa  yanayofanya biashara ya  kanda  hiyo  linalojulikana  kama Intergovernmental Authority on Development , IGAD, ama  mamlaka ya ushirikiano  wa  serikali katika  maendeleo, hadi  sasa zimeshindwa  kuleta  amani ama  hata  makubaliano ya muda  mrefu ya  kusitisha  mapigano.
 

Mazungumzo  ya  mwisho  yameshuhudia  makubaliano  mengine  ya kusitisha  mapigano  wakati  mapendekezo, ikiwa  ni  pamoja  na kugawana  madaraka na  Machar kurejea  katika  wadhifa  wake  wa makamu  wa  rais, bado  yanajadiliwa.

Wasudan kusini  milioni  saba, zaidi  ya  nusu ya  idadi  jumla  ya wakaazi  wa  nchi  hiyo, watahitaji msaada  wa  chakula  katika mwaka  huu 2018, kwa  mujibu wa  Umoja  wa  mataifa.

Wakati  huo  huo baraza  la  Usalama la  Umoja  wa  mataifa linatarajiwa  kupiga  kura  wiki  hii kuweka  vikwazo vya  silaha  dhidi ya  Sudan kusini, ikiwa  ni pendekezo  la  Marekani ambalo  linafuatia makubaliano  ya  kugawana  madaraka  baina  ya  viongozi  hao wawili  wanaogombana.
 

Südsudan - Kindersoldaten
Wapiganaji watoto katika mzozo wa Sudan kusiniPicha: Getty Images/AFP/C. Lomodong

Marekani  ni mfadhili  mkuu  wa  misaada  kwa  Sudan kusini, na ilikuwa  muungaji  mkono  mkuu  wa  uhuru  wa  nchi  hiyo uliopatikana mwaka  2011.
 

Lakini  uvumilivu wa washirika  wa kigeni  wa  Sudan  kusini umekwisha  baada  ya  juhudi  kadhaa  kushindwa  kuleta  amani nchini  humo, ambayo  hivi  sasa  imo  katika  mwaka  wa  nne  wa vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe vinavyolenga mauaji  ya kikabila, ubakaji  wa  makundi pamoja  na  madhila  mengine yanayotokea.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef