1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CCM chadhibiti Dar es Salaam baada ya uchaguzi

George Njogopa29 Oktoba 2020

Matokeo ya ubunge katika jiji la Dar es Salaam lililokuwa ngome kuu ya upinzani kwa miaka mitano iliyopita yanaonyesha kuwa jiji hilo sasa limerejea kwenye chama tawala CCM. 

https://p.dw.com/p/3kbZj
Skyline Dar es Salaam, Tansania
Picha: DW/Eric Boniphace

Dar es salaam ambayo ni kitovu cha kibiashara na jiji la bandari limegeukia upande mwingine upande ambao unatafsiri siasa mpya zinazoendelea kushuhudia sasa nchini kote kutokana na matokeo yanayoendelea kutangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi kufuatia uchaguzi wa siku ya Jumatano.

Matokeo yaliyojulikana hadi sasa, chama tawala kimejizolea ushindi mkubwa katika maeneo mengi na hivyo kulikumbatia tena jiji hili linalokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 6,000 ambalo pia limeshuhudia katika miezi ya hivi karibuni likiongezeka wilaya za kiutawala zinazofikia tano kutoka tatu zilizokuwa kwa miaka mingi.

Chama hicho kimeyabakiza mikononi mwake majimbo yake ya awali kama yale ya Kigamboni, Ilala na Segerea ambayo katika uchaguzi uliopita hayakubebwa na upepo uliosukumwa na nguvu ya Ukawa ulioundwa na muungano wa vyama vitatu vyenye nguvu.

Wakati upepo huo ulipoanza kupoteza mwelekeo, chama hicho kilifanikiwa pia kuyarejesha baadhi ya majimbo kama yale ya Kinondoni na Ukonga yaliyokuwa upinzani kabla ya waliokuwa wabunge wake kujiondoa upinzani na kujiunga na CCM katika kile kilichojulikana kama kuunga mkono juhudi.

Katika uchaguzi wa jana majimbo hayo yote yameendelea kusalia CCM. Matokeo hayo yanatoa mwelekeo mpya kuhusu siasa za jiji hili na kama anavayosema mmoja wa wakazi wake ushindi huo wa CCM ni sehemu ya kudhihirisha namna chama hicho kilivyokua kimejipanga kurejesha himaya yake.

Wapiga kura wapiga mlolongo kituoni kupiga kura Dar es Salaam 28.10.2020
Wapiga kura wapiga mlolongo kituoni kupiga kura Dar es Salaam 28.10.2020Picha: Ericky Boniphace/DW

Chama hicho pia kimeshinda katika majimbo mengine ikiwamo lile la Segerea ambalo aliyekuwa mbunge wake alijutupa katika jimbo la Tarime Vijijini na kumshinda mtetezi wake John Heche wa Chadema. Hali kama hiyo imejitokeza pia katika Jimbo la Mbagala ambalo wakati fulani limewahi kuwa ngoma ya CUF.

Chama hicho tawala kinajivua kuwa na usemi mkubwa katika majimbo ya uchaguzi ya Dar es salaam lakini baadhi ya wananchi waliopiga kura katika uchaguzi huo wa jana wanasema hakipaswi kusherekea ushindi huo.

Hali ya vuta nikuvute ilikuwa ikitupiwa macho katika majimbo ya Ubungo na Kawe na baadhi ya duru za habari zilisema CCM ilikuwa mbioni kushinda majimbo hayo ingawa hadi ripoti hii ikiandaliwa matokeo rasmi yaliyokuwa bado kutangazwa.

Jimbo la Kawe linatajwa kuwa moja ya jimbo muhimu kwa pande zote mbili kutokana na namna lilivyobeba ushindani kwa wagombea wake, Halima Mdee na Joseph Gwajima.

Upinzani unasema uchaguzi wa mwaka huu ulitawaliwa na visa vya udanganyifu kama vile kuwepo kwa masanduku bandia ya kura yaliyokua yakiingizwa katika vituo vya kupigia kura huku mawakala wake wakitishwa na kukataliwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.

Tume ya taifa ya uchaguzi imesema haijapokea taarifa rasmi kuhusu madai hayo na hivyo imetaka wananchi kuyapuuza, ingawa upinzani umekuwa ukionyesha baadhi ya karatasi zinazodaiwa zilighushiwa wakati wa upigaji wa kura.