1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yapiga hatua katika njia nzuri asema Leila Zerougui

Saleh Mwanamilongo
21 Januari 2021

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepiga hatua nzuri licha ya kuendelea kuwepo na makundi ya wapiganaji,amesema kiongozi wa Monusco anayemaliza muda wake.

https://p.dw.com/p/3oE2u
Leila Zerrougui
Picha: picture-alliance/epa/M. Trezzini

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepiga hatua nzuri licha ya kuendelea kuwepo na makundi ya wapiganaji, amesema kiongozi wa Monusco,Leila Zerougui ambae amemaliza muda wake nchini Congo. Lakini nchini humo mashirika ya kiraia na baadhi ya wanasiasa wanamaoni mseto kuhusu muhula wa Leila nchini Congo. 

Leila Zerougui,kiongozi wa kikosi chakulinda amani cha Umoja wa Mataifa, Monusco, amesema Congo bado inakabiliwa na mzozo, lakini mzozo huo umeshughulikiwa kwenye majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo.

''Mafanikio mengi yamefikiwa''

 Kwenye mkutano wake wa mwisho na wandishi habari nchini Congo, Zerougui amesema kwamba Congo bila shaka imepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

 ''Congo ni inchi yenye uwezo wa kujiendeleza. Mafanikio mengi yamefikiwa wakati wa muhula wangu. ikiwemo kisiasa, leo tuna rais wa zamani Joseph Kabila, tuna rais wa sasa, tuna wanasiasa wakuu Jeanpierre Bemba, Moise Katumbi Martin fayulu wote wako nchini, Hilo halingewezekana miaka ya nyuma''

Leila Zerougui amewatolea mwito raia wa Congo kuwa na matumaini juu ya nchi yao na kufanya kazi ili kudumisha amani.

Mjumbe huyo maalumu wa umoja wa mataifa nchini Congo amemaliza muhula wake wa miaka mitatu  kama kiongozi wa Monusco. Amesema sio rahisi kukamilisha kila kitu , na mengi yamebaki kufanywa ilikuwepo na amani ya kudumu kote nchini.

Maoni mseto kuhusu muhula wa Bi Zerrougui

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo,MONUSCO
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo,MONUSCOPicha: Reuters/File Photo/O. Oleksandr

Kikosi cha Monusco kilichomo nchini Congo toka miaka 21 sasa kimekuwa kikilaumiwa kushindwa kurejesha amani hasa huko mashariki mwa Congo.

Wanasiasa na mashirika ya kiraia wanamaoni mseto kuhusu muhula wa miaka mitatu wa Bi Leila Zerougui nchini Congo. Baadhi wamemkosoa na kusema hakufanikisha amani kurejea huko kwenye majimbo ya Kivu na vilevile kisiasa alifumbia macho udanganyifu wa uchaguzi wa mwaka 2018.

Hata hivyo Dieudonné Mushagalusa mratibu wa mashirika ya kiraia mjini Kinshasa amesema kwamba Leila alijitahidi kuliko baadhi ya watangulizi wake.

''Tunafikiri alifanya alichoweza. Kwa sababu huko Kivu na maeneo mengine usalama kuna usalama mdogo kwa siku nyingi, na yeye hawezi kumaliza hali hiyo mara moja.''

Desemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, liliongeza kwa kipindi cha miezi 12 muhula wa kikosi cha Monusco. Na wiki iliopita Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa alimteuwa Bintu Keita kutoka Guinea kuwa kiongozi mpya wa kikosi cha Monusco nchini Congo.