1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire ku moto

1 Aprili 2011

Mapigano makali yanaendelea nchini Cote d'ivoire kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono Alassane Ouattara na wanajeshi wale wanaomtii Laurent Gbagbo.

https://p.dw.com/p/10lsB
Moshi mzito katika majengo ya Abdijan
Moshi mzito katika majengo ya AbdijanPicha: dapd

Milio ya risasi na makombora imesikika hii leo karibu na makaazi ya Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madaraka nchini Cote d'Ivoire pamoja na kasri lake.

Mkaazi mmoja wa eneo la Cocody ambako Gbagbo anaishi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa milio hiyo ya risasi imekuwa ikiendelea kwa muda na wanajeshi watiifu kwa Gbagbo wamekwamia katika maeneo yao.

Makabilianio makali baina ya wanajeshi watiifu kwa Rais huyo anayeondoka na jeshi la Rais anayetambulika kimataifa Allasane Ouattara yalianza hapo jana karibu saa nne usiku karibu na boma lake Laurent Gbagbo.

Imeripotiwa kuwa Gbgbo mwenyewe hakuwa nyumbani kwake wakati huo. Wanajeshi wa Ouattara waliingia katika mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan, hapo jana Alhamisi baada ya kuifagia miji mingine ya nchi hiyo huku wakikabiliana na vikosi vya Gbagbo. Usiku wa kuamkia leo waliutwaa uwanja wa ndege pamoja na kituo cha runinga ya kitaifa.

Raia wakikimbia mapigano nchini Cote d'Ivoire
Raia wakikimbia mapigano nchini Cote d'IvoirePicha: AP

Mapigano yaliendelea hii leo katika wilaya ya Plateau ambayo ni ngome ya kasri lake Gbagbo ambako miliyo ya risasi na makombora mazito ilitanda hewani.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa takribani wanajeshi 50,000 wameziwacha nyadhifa zao na kwamba ni wale tu walio katika kundi la Republican Guard linalomuunga mkono Gbagbo na wanafunzi waliojihami ambao ni kiasi ya 2,000 waliosalia katika vita ili kuyalinda makaazi ya kiongozi huyo.

Kiasi ya raia wa kigeni 500 walikimbilia hifadhi katika kituo cha kijeshi cha Ufaransa mjini Abidjan. Haya ni kwa mujibu wa chombo kimoja cha habari cha Kifaransa.

Ufaransa ina vikosi vyake nchini Cote divoire katika operesheni ya kulinda amani. Cote divoire ilitumbukia katika wimbi la machafuko baada ya Gbagbo kukataa kumwachia madaraka hasimu wake Alassane Ouattara baada ya uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka jana ambao Umoja wa Mataifa unasema Rais huyo alishindwa.

Hata hivyo makabiliano makali ya kijeshi na wanajehsi waasi wanaomuunga mkono Ouattara yalizuka wiki kadhaa zilizopita baada ya juhudi za upatanishi na vikwazo kushindwa kumfanya Gbagbo kusalimu amri.

Vikosi vya Ouattara vimelitwaa eneo la Yamoussoukro, ambalo ndio mji mkuu wa kisiasa nchini humo na pia mji wa San Pedro, ambayo ni bandari kubwa zaidi ya kuuza kakao ulimwenguni.

Msemaji wa Ouattara Patrick Achi amesema kuwa waasi tayari wamekitwaa kituo cha kitaifa cha runinga ambacho kimekuwa kikitangaza propaganda za kumpigia debe Gbagbo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri:Josephat Charo