1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo dhidi ya kakao la Cote d'Ivoire vyawaumiza wakulima

16 Machi 2011

Marufuku ya jumuiya ya kimataifa dhidi ya kakao kutoka Cote d'Ivoire kwa nia ya kumdhibiti rais anaeng'ang'ania madaraka, Laurent Gbagbo, imesababisha shehena kwa shehena za zao hilo kurundikana kwenye ghala za wakulima.

https://p.dw.com/p/10aQp
Laurent Gbagbo
Laurent GbagboPicha: picture alliance / dpa

Taarifa zinaonesha kuwa, sio tu kwamba ubora wa kakao lililo kwenye mikono ya wasafirishaji unapotea, lakini pia zao hilo linauzwa katika masoko yasiyo rasmi au kwa njia ya panya kwa gharama ya chini kupita kiasi.

Hali ya kibiashara kwa wasafrishaji hawa imekuwa si nzuri kutokana na vurugu za kisiasa nchini humo.

Majeshi ya Laurent Gbagbo yamekuwa yakivamia katika baadhi ya mitaa mjini Abidjan ambayo imeonekana kuwa na wafuasi wa mpinzani wake, Alassane Ouattara.

Kwa mara ya kwanza, majeshi yametumia helikopta katika jitihada za kuyadhibiti maeneo yanayomuunga mkono Ouattara, kama vile Abobo.

Alassane Ouattara
Alassane OuattaraPicha: AP

Umoja wa Ulaya umeweka kikwazo cha kutonunua kakao kutoka nchi hiyo ili kumfanya Gbagbo awe na wakati mgumu kifedha za kigeni. Lakini matokeo ya hatua hiyo yanawaneemesha wengine, hasa nchi jirani, hata zile ambazo hazilimi kabisa zao hilo, kama vile Mali, Burkina Faso na Togo.

Katikati ya Februari mwaka huu, zaidi ya tani 400,000 za kakao zilizuiwa katika bandari za Abidjan na San Pedro, wakati zikiwa katika hatua ya kusafirishwa katika nchi za Ulaya.

Msafirishaji mmoja wa zao hilo kutoka mashariki mwa Cote d'Ivoire, Adrien, amesema kila kukicha kakao linaoza kutokana na kukaa kwa muda mrefu katika mazingira mabaya.

Adrien amesema hali ndio imekuwa hivyo na kwamba hana la kufanya kutokana na athari za mgogoro wa kisiasa ambao umeikumba nchi hiyo iliyowahi kutajwa kama lulu ya Magharibi mwa Afrika.

Mwanamke wa Cote d'Ivoire akiiombea nchi yake amani
Mwanamke wa Cote d'Ivoire akiiombea nchi yake amaniPicha: picture alliance/dpa

Mfanyabishara hiyo mwingine mkubwa wa zao, Blandine Gloudoueu, amelalamika kushindwa kununua tani 35 za kakao kwa kiasi cha dola 50,000 za Kimarekani.

Gloudoueu amesema hiyo ni ishara ya kuanza kufilisika kibiashara na kuhofia namna gani kama mkazi wa kawaida ataweza kuhudumia familia yake yenye watu 20.

Naye Rais wa Ushirika wa Wakulima wa Cote d'Ivoire, Joseph Koume Yao, amesema inashangaza kuona kwamba Mali hivi sasa inajitangaza kuzalisha hadi tani 100,000 wakati 2004 ilikuwa tani elfu nane tu.

Taarifa ya Shirika la Habari la Uingereza, BBC, imesema kuwa inakadiriwa zaidi ya tani 170,000 zimehamishwa kutoka Cote d'Ivoire kwa njia haramu, tatizo ambalo limesababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 34 za Kimarekani.

Yao anathibitisha taarifa hizo kwa kusema kuwa, wiki chache zilizopita wafanyabiashara walijinunulia zao hilo kwa bei ya kutupa na kusafirisha kwa njia ya panya.

Yao ameongeza kuwa, hali ni mbaya nchini mwao kwa kuwa mchezo kama huo unainufaisha Ghana ambayo ni mahasimu wao wakubwa katika biashara ya kakao.

Cote d'Ivoire inakadiriwa kuzalisha tani milioni 1.2 ya zao la kakao kwa mwaka ambayo inalipatia taifa hilo kiasi cha asilimia 48 ya pato lake la taifa.

Mwandishi: Sudi Mnette/IPS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman