1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deutsche Welle: Makala ya Afrika Wiki hii

19 Februari 2010

<p>Karibu katika makala nyengine ya Afrika wiki hii, Uchambuzi wa baadhi ya yale muhimu yaliotokea Afrika mnamo juma hili.

https://p.dw.com/p/M63S
Picha: picture alliance/akg Images
Miongoni mwayo ni hali ya kisiasa nchini Kenya, kukizuka mvutano mwengine kati ya pande mbili zinazounda serikali ya Muungano nchini humo -kikao cha halmashauri kuu ya chama tawala  nchini Tanzania CCM chamalizika , kikitoa  sura ya mustakbali wake Ivory Coast nayo yaingia katika mgogoro mwengine wa kisiasa na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atoa wito vikwazo dhidi ya nchi yake viondolewe.

Lakini kwanza tunaanzia na kile kilichogonga vichwa vya habari Juma hili, ambacho ni mapinduzi ya kijeshi nchini Niger dhidi ya rais

Mamadou Tandja, ambaye mwaka jana alizusha hali ya wasi wasi kutokana na majaribio yake ya  kung'ang'ania madaraka, alipoibadili katiba na kuitsha kubadili kifungu cha mihula miwili ya uongozi.

Präsident der Republik Niger, Mamadou Tandja
Rais Mamadou TandjaPicha: AP Photo

Wanajeshi walioasi waliivamia Ikulu ambako rais huyo alikuwa na mkutano na baraza la  mawaziri. Kulizuka milio ya risasi na moshi ukionekana  kufuka katika jengo hilo la Ikulu. Kulikuwa na hali ya mtafaruku kwa  muda wa masaa kadhaa, kabla ya Kanali Goukoye Abdul Karimou kujitokeza  kwenye televisheni na kuliarifu taifa kwamba rais Tandja amepinduliwa. Alisema Baraza kuu kwa ajili ya kurejesha demokrasi nchini Niger limeisimamisha katiba na kuzivunja taasisi zote.

Taarifa ya Kanali huyo kama msemaji wa baraza hilo ilitolewa akiwa amezungukwa na wanajeshi wenzake. Rais Tandja  alikuwa akizuiliwa katika kambi moja ya kijeshi mjini Niamey.

Jumuiya ya uchumi ya Afrika magharibi  ECOWAS, iliisimamisha uanachama Niger baada ya  Tandja kuibadili katiba na kujiongezea muda wa madaraka kwa kuitisha uchaguzi uliosusiwa na vyama vya upinzani. Marekani na Umoja wa Ulaya pia vikaiwekea vikwazo nchi hiyo.  Taarifa ya Marekani baada ya mapinduzi hayo ya Alhamisi ilisema wakati inalaani  utwaaji madaraka kwa nguvu, ina matumaini kwamba Niger itarejea haraka katika utawala wa kidemokrasi.

Katika eneo la Mashariki mwa bara hilo la Afrika, huko nchini Kenya pande  mbili zinazounda serikali ya muungano nchini Kenya zimeingia katika  mgogoro mpya wiki hii, baada ya Jumapili iliopita, Waziri mkuu Raila Odinga kuwasimamisha kazi mawaziri wawili , William Ruto waziri wa kilimo na  mwenzake wa elimu Sam Ongeri hadi utakapomalizika uchunguzi  juu ya shutuma za rushwa zinazowakabili. Lakini muda mfupi baadae Rais Mwai Kibaki akasema hatua hiyo si halali kwa msingi wa kwamba Bw Odinga hana mamlaka hayo,pamoja na kwamba  Waziri mkuu huyo anasema ni yeye anayeongoza shughuli za serikali.

Kutokana na  mvutano huo ambao umetaoa sura paia ya  kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya chama cha ODM cha  Bw  Raila ambacho Bw Ruto ni miongoni mwa vigogo wa chama hicho, ODM ikasema itasusia vikao vyote vya baraza la mawaziri.

Kenia Bekanntgabe des Kabinetts Odinga hinter Kibaki
Rais Kibaki na Raila OdingaPicha: AP

Wakati  Mudavadi akitangaza hayo,  mbunge wa Mombasa na Waziri wa utalii ambaye pia ni mwanachama wa ngazi ya juu katika ODM Bw Najib Balala akizungumzia kadhia hiyo alisema:-

Ama katika kile kilichoonekana  kuwa ni kujibu kitisho cha ODM, chama cha PNU mshirika  katika serikali ya  mseto, kikatoa taarifa yake mjini Nairobi. Mwandishi wetu mjini humo  Alfred Kiti  alituarifu zaidi.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa barani Afrika , wameonya kuhusu uwezekano wa mvutano huo  kati ya ODM na PNU kuwa mkubwa zaidi na hatari ya kuzuka tena machafuko pindi ukipamba moto. Waziri mkuu Raila Odinga kwa upande amemuomba Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Koffi Annan aliyekuwa mpatanishi wa mgogoro uliozuka  baada ya uchaguzi 2007 na kusababisha pande hizo hatimae kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya  muungano, aingilie kati mvutano huu mpya akisema  rais Kibaki anaweka vikwazo vya kutekelezwa makubaliano yaliofikiwa.

Pamoja na hayo  kulipatikana taarifa siku ya Alhamisi kwamba viongozi wa ODM na  PNU watakutana Jumapili hii kutafuta suluhisho la mgogoro huo. Akithibitisha  hayo katika mahojiano na  DW, Katibu mkuu wa ODM Profesa Peter Anyang Nyo´ngo alisema.

Katika nchi jirani na Kenya-Tanzania, chama tawala CCM kilimaliza kikao chake cha halmashauri kuu ya taifa mjini Dodoma kilichoitishwa kuzungumzia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mvutano kati ya makundi mawili chamani huku moja likisema linapigana dhidi ya ufisadi, na pia hali ya kisiasa  visiwani Zanzibar, kufuatia  makubaliano ya  kuondoa uhasama kati ya CCM Zanzibar na chama cha upinzani CUF, kukiwa na uwezekano hatimae wa kuundwa serikali ya mseto. Katika suala hilo, kumezungumzwa na bado kunazungumzwa mengi. Hata hivyo  Mwenzangu Othman Miraji alizungumza  na  Katibu wa uenezaji na itikadi wa CCM Bw John Chiligati ambaye kwanza  alikaua na haya ya kueleza  kuhusu matokeo ya kikao hicho cha Dodoma.

Tunarudi tena Afrika  magharibi ambako  rais  Blaise Compaore wa Burkina Faso alitoa wito wa kuanza tena maandalizi ya uchaguzi nchini Ivory Coast, baada ya ghafla rais Laurent Gbagbo kulivunja baraza la mawaziri na tume ya uchaguzi, tukio ambalo bila shaka huenda likachelewesha uchaguzi uliopangwa  mwezi ujao wa Machi.

Blaise Compaore
Rais Blaise Compaore wa Burkina FasoPicha: AP

Rais Compaore alikuwa mpatanishi kati ya pande zinazohasimiana huko Ivory Coast ambazo zilifikia makubaliano 2007 hasa baina ya waasi wa kaskazini wanaolidhibiti bado eneo hilo  pamoja na wapinzani wa kiraia upande mmoja na serikali iliokuweko wakati huo chini ya uongozi wa rais wa sasa  Laurent Gabagbo.

Taifa hilo lenye utajiri wa  zao la Cocoa na wakati mmoja likitajwa kama lulu ya Afrika  lilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002-2003 vikiligawa pansde mbili kaskazini na kusini.

Rais Campaore pia ametoa wito wa kuundwa haraka serikali mpya itakayozihusisha pande zote husika, huku akiwaomba waivory Coast kuwa  watulivu na wastahamilivu.

Wakati hayo yakitokaea huko Ivory Coast jirani yake katika eneo hilo Guinea ilifungua ukurasa mpya kuelekea  demokrasia, baada ya kuundwa serikali ya mpito. Serikali hiyo  inaongozwa na Waziri mkuu wa kiraia  Jean Marie Dore akiwa ni ya watu 39  mchanganyiko wa raia na wanajeshi. Miongoni mwa  mawaziri wake hata hivyo ni wanajeshi wawili wanaohusishwa na mauaji ya  septemba mwaka jana  dhidi ya waandamanaji  zaidi ya 150 wa upinzani waliokusanyika katika uwanja wa michezo mjini Conakry kudai demokrasia. Hao ni Kapteni Claude Pivi na Luteni Kanali Moussa Tiegboro.

Pivi pia anabakia kuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais wakati Toegboro pia mnaendelea na wadhifa wake wa  kukiongoza kikosi cha kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu.

Watatezi wa haki za binaadamu wamepinga kuteuliwa wanajeshi hao wawili wakisema ni fedheha.

Kiongozi wa taifa anaendelea kuwa Jenerali Sekouba Konate aliye kaimu  wadhifa huo baada ya  kupigwa risasi Kapteni Moussa Dadis Camara na mmoja wa walinzi wake  ambaye hadi sasa hajulikani aliko katika jaribio la kumuuwa mwezi Desemba mwaka jana . Camara anaendelea na matibabu nchini Burkina faso baada ya kutibiwa hapo awali huko Morocco.

Katika eneo la maziwa makuu,

Wawakilishi wa serikali za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na wale wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, walikutana  Kigali mapema wiki hii, kujadiliana jinsi ya kufikia makubaliano ambayo yatafungua ni kwa wakimbizi wa nchi hizo mbili kurejea makwao kwa hiari yao.

Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Rwanda, ambao wakimbilia eneo la mashariki mwa kongo, huku Rwanda nayo ikiwahifadhi maelfu pia ya wakimbizi wa Kongo waliyoko katika kambi ya Gihembe wilayani Gicumbi. Mwandishi wetu mjini Kigali Daniel Gakuba alitutumia ripoti.

Tunamalizia kusini mwa Afrika ambako Robert Mugabe wa Zimbabwe alitamka  mnamo siku ya Jumatano kwamba yeye pamoja na washirika wake katika serikali ya mseto nchini humo akimaanisha chama cha upinzani MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai na tawi lililojitenga  MDC  ya Athur Mutambara wamekubaliana kwamba vikwazo vinapaswa kuondolewa. Matamshi yake yalikuja siku moja baada ya Umoja wa ulaya kurefusha kwa miezi 12 mengine  hatua yake ya kuwapiga marufuku masahibu kadhaa wa Mugabe kuingia katika nchi 27 wanachama wa Umoja huo, na kuzuwia mali za Mugabe na  maafisa wake wapatao 100.

Robert Mugabe November 2008
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: picture-alliance/ dpa

Pamoja na hayo akizungumzia uamuzi wa Umoja wa Ulaya , Rais Mugabe alisema hashangazwi akiongeza " Tunajua msimamo wao, hawataki mtu yeyote au nchi yoyote duniani kupiga hatua ya maana ya maendeleo. Uhusioano baina ya  Zimbabwe na Umoja wa Ulaya umezorota kwa karibu miaka 10, ikitokana na machafuko yanayohusiana na uchaguzi na madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu wa serikali ya Mugabe na chama chake cha Zanu-PF, ambayo mara nyingi hufungamanishwa na  mpango wa mageuzi ya ardhi uliowalazimisha wazungu kutoa sehemu kubwa ya ardhi zao za kilimo kwa serikali iliodai kwamba ni kuwagawia waafrika wasio na ardhi. Lakini kumekuweko na malalamiko makali  kwamba  mashamba mengi yamechukuliwa na  vigogo  na wapambe wa rais Mugabe.

Mwandishi:Abdul-Rahman,Mohammed /Reuters/AFP/Correspondents

Mhariri: Miraji Othman