1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djotodia ahalalisha utawala wake Jamhuri ya Afrika ya Kati

14 Aprili 2013

Michel Djotodia, ambae muungano wake wa waasi wa Seleka ulichukua madaraka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi uliyopita, amechaguliwa siku ya Jumamosi kuwa rais wa mpito nchini humo na baraza la taifa la mpito.

https://p.dw.com/p/18FY8
Rais Michel Djotodia.
Rais Michel Djotodia.Picha: Getty Images

Djotodia aliejitangazia urais baada ya vikosi vyake kuchukua udhibiti wa mji mkuu Bangui Machi 24, alikuwa mgombea pekee katika kura hiyo iliyofanyika mwanzoni mwa kikako cha kwanza cha baraza hilo. Rais wa mpito atatawala kw akipindi kisichopungua miezi 18, wakati ambapo baraza hilo la mpito lenye wanachama 105 litachukua nafasi ya baraza la katiba. Baraza hilo linajumuisha maafisa wa Seleka, wajumbe wa utawala uliondolewa na vile vile wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Michel Djotodia wakati akiwa kiongozi wa waasi wa Seleka.
Michel Djotodia wakati akiwa kiongozi wa waasi wa Seleka.Picha: picture-alliance/ap photo

Mwanadiplomasia moja aliezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina lake, aliitaja kura hiyo kamam hatua iliyohitajika kuupa uhalali utawala wa Djotodia. Majirani wa Jamhuri ya Afrika ya kati na washirika wa magharibi wameonya kuwa wasingetambua utawala wa Djotodia, lakini pia hawaonyeshi nia ya kuunga mkono kurejea kwa kiongozi aliepinduliwa, Francois Bozize.

Ni taarifa kidogo tu zinazofahamika kuhusu kiongozi huyo mpya wa taifa hilo lisilo na pwani, lililo na utajiri mkubwa sana wa madini, ambao hata hivyo haujaguswa, na linaendelea kuwa moja ya mataifa maskini zaidi duniani. Baada ya miaka kadhaa kama mtumishi wa umma na mwandiplomasia, Djotodia aliepata mafunzo yake nchini Urusi, ambae alizwaliwa mwaka 1949, aligeukia uasi na kuanzisha vuguvugu la kijeshi mwaka 2005, m iaka miwili baada ya Bozize kuchukua madaraka kupitia mapinduzi.

Changamoto zinazomkabili

"Nafahamu umuhimu wa kazi mlioniamini kuifanya. Nitafanya kila juhudi kuhakikisha ufanisi wa serikali ya mpito ambayo imeanza kazi yake hivi sasa," Djotodia alisema katika hotuba yake rasmi ya kwanza kama kiongozi siku ya Jumamosi. Alisema changamoto ambazo atakabiliana nazo katika miezi michache ijayo ni pamoja na kujenga upya umoja wa kitaifa, kuhakikisha usalama nchini kote, kurejesha amani ya kijamii na kufufua uchumi.

Mashambuli za muungano wa Seleka yalioanza Disemba mwaka jana yalisababisha machafuko na uporaji ambavyo hadi sasa havijaweza kudhibitiwa. Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo ina ukubwa sawa na Ufaransa, lakini yenye wakaazi milioni tano tu, imejaa silaha na utulivu unaonekana kuikwepa nchi hiyo, ambako serikali kuu imekuwa ikipambana mara kwa mara kuweka mamlaka yake nje ya mji mkuu.

Michel Djotodia (kushoto) akishikana mkono na rais aliempindua Francois Bozize, wakati wa mazungumzo ya amani mjini Lebreville Januari mwaka huu.
Michel Djotodia (kushoto) akishikana mkono na rais aliempindua Francois Bozize, wakati wa mazungumzo ya amani mjini Lebreville Januari mwaka huu.Picha: dapd

Mapinduzi ya Djotodia pia yalisababisha wasiwasi wa kidini na wakristu wengi wanahofia kuwa utawala unaodhibitiwa na waasi kutoka kaskazini mwa nchi hiyo unaweza kulaazimisha Uislamu nchini kote. Kiongozi huyo wa waasi ndie kiongozi wa kwanza Muislamu wa taifa hilo lililo na Wakristu wengi. Djotodia amesisitiza kuwa ataendelea kuwa muaminifu kwa kanuni za makubaliano ya amani ya Januari 2013, yaliyofikiwa kati ya muungano wa Seleka na utawala wa Bozize.

Awali kiongozi huyo alitangaza kuwa angetawala kwa amri kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, lakini jumuiya ya kimataifa ilishinikiza kuwekwa taasisi za mpito na ratiba inayobana. Kura ya Jumamosi inatazamiwa kuirudisha Jamhuri ya Afrika ya kati katika msitari, baada ya Umoja wa Afrika kuisimamisha uanachama na wafadhili kusitisha misaada kwake. Jamhuri ya Afrika ya Kati inategemea zaidi msaada kutoka nje.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe
Mhariri: Sudi Mnette