1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Chama tawala UDPS chasema maandamano kuendelea

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.10 Julai 2020

Chama kilichopo madarakani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, UDPS, kimesema wakongomani wataendelea na maandamano hadi madai yao yasikike na kuwepo na mabadiliko nchini humo.

https://p.dw.com/p/3f642
Demonstrationen gegen die Präsidentschaftspartei Union für Demokratie und sozialen Fortschritt (UDPS) in Kinshasa
Picha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Haya yanajiri baada ya watu kadhaa pamoja na askari polisi kuuawa katika makabiliano kati ya waandamanaji na polisi.

Baada ya maandamano yaliyoyafanya Alhamisi katika miji mbalimbali ili kupinga uteuzi wa Ronsard Malonda kama mwenyikiti wa tume huru ya uchaguzi, na ambamo watu watatu waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, chama hicho kimesema kitamshinikiza pia waziri wa mambo ya ndani ajiuzulu kutokana na kushindwa kuisimamia polisi.

Katibu mkuu wa Chama cha Muungano wa Demokrasia na Maendeleo ya Jamii, UDPS, Augustin Kabuya, ameelezea kuhuzunishwa na vifo vya wanachama watatu wa chama hicho katika maandamano ya Alhamisi, moja kutoka hapa Kinshasa na wawili mjini Lubumbashi, kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Je kuna udhaifu wa wizara ya mambo ya ndani?

Kwa mjibu wa katibu mkuu huyo, inaonekana wazi kwamba waziri wa mambo ya ndani licha ya kuwa ni mmoja wa wanachama wa UDPS, hajafaulu kuisimamia polisi na ndiyo maana siku za usoni, itambidi kuachishwa kazi.

Waandamanaji wakiwa karibu na pikipiki inayoteketea moto mjini Kinshasa 09.07.2020
Waandamanaji wakiwa karibu na pikipiki inayoteketea moto mjini Kinshasa 09.07.2020Picha: Getty Images/AFP/A. Mpiana

Ronsard Malonda kutoka muungano wa makanisa hapa nchini alidhibitishwa na bunge la taifa wiki iliyopita, kama mwenyikiti mpya wa tume huru ya uchaguzi ili kuichukuwa nafasi ya Corneille Nangaa, lakini anapingwa vikali na wengi kutokana na historia yake ya kuwa katibu mtendaji wa timu yake Corneille Nangaa ambayo ililalamikiwa kwa kutoa matokeo yasiyoridhisha.

Chama hicho cha rais Felix Tshisekedi kimesema wakongomani wataendeleza maandamano na kumuomba rais asimkubali Malonda kuiongoza tume hiyo, kwani wanataka sasa mabadiliko ili chaguzi zitakazofanyika zikubaliwe na wote.

Wito watolewa wa kutaka tume ya uchaguzi kuwa huru

Yusuf Mabanze ambaye ni mmoja wa viongozi wa UDPS amesema: "Inabidi wasimamizi wa uchaguzi ama CENI, wawe watu huru ili matokeo yasipingwe na mtu hata moja. Tunaona Ronsard Malonda yeye ni mwanachama wa FCC, kikundi cha bwana Kabila. Na yeye akaiongoza CENI, matokeo yataletea inchi yetu vurugu na changamoto. Tunataka uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uwe unaheshimika ulimwengu nzima."

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix TshisekediPicha: G. Kusema

Wengi miongoni mwa wachambuzi wa mambo hapa nyumbani wanashangazwa kuona kila mara UDPS inawamwaga wafuasi wake mitaani kwa maandamano, ingawa chama hicho ndicho kipo madarakani.

Kabasubabu Katulondi ambae ni mwandishi pia mchambuzi wa mambo ya kisiasa ameiambia DW, kuwa chama hicho kinawachanganya wengi kwani kinaonekana kipo madarakani bila kuacha upinzani. 

"Inaonekana UDPS ipo madarakani na katika upinzani. Licha ya kuwa UDPS na FCC wanaongoza pamoja, tuliona wafuasi wa UDPS wanapinga musuada wa mabadiliko ya sheria, wakaandamana na kuvunja majumba ya watu. Tuliowaona pia wakiwazuia wabunge kuingia bungeni." Amesema Katulondi.

Serikali imekataza maandamano yote kwa sababu ya janga la covid-19 linaloikumba nchi hii, ila hatua hiyo bado haijaheshimiwa. Maandamano mengine yanaandaliwa wiki ijayo na upinzani pia harakati mbalimbali za kutetea wanainchi.

Mwandishi: Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.

Mhariri: Iddi Ssessanga