1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan anasema Uturuki itasimama kidete kutetea haki zake

Saleh Mwanamilongo
26 Agosti 2020

Rais wa Uturuki Recep Erdogan amesema kwamba Uturuki itasimama kidete kutetea haki zake za Bahari ya Mediterania,huku akiIhimiza Ugiriki kuepuka mzozo.

https://p.dw.com/p/3hYGI
Türkei Erdgas Schwarzes Meer Bohrschiff Fatih
Picha: Reuters/Presidential Press Office

Rais wa Uturuki; Recep Tayyıp Erdogan amesema kwamba Uturuki itasimama kidete kutetea haki zake za Bahari ya Mediterania, huku akiIhimiza serikali ya Ugiriki kuepuka mzozo.

''Kamwe hatuwezi kuweka hatarini kilicho chetu'', alisema  Erdogan kwenye sherehe ya maadhimisho ya kumbukumbu ya vita vya mwaka 1071 baina ya Waturuki wa Seljuk na Himaya ya Byzantine huko Manzikert kwenye jimbo la kusini mashariki la Mus.

Erdogan amesema Uturuki iko tayari kufanya kila liwezekanalo kuchukuwa haki yake iliopo katika Bahari ya Mediterania, pia Bahari ya Egean na Bahari Nyeusi. Ameiomba Ugiriki kubaki kando ya mzozo huo.

Jumatano, Waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis alisisitizia nia ya kuWeko na mazungumzo baina ya nchi yake na Uturuki kuhusu mipaka ya eneo maalum la kiuchumi kwenye eneo la mashariki la Mediterania.

Wakati huo huo; Mitsotakis aliwaambia wabunge wa nchi yake kwamba Ugiriki italitanua mara mbili eneo lake la majini. Kauli hizo za Uturuki na Ugiriki zimetolewa licha ya juhudi za Ujerumani za kutaka suluhisho la mzozo wa Mediterania.

Miito ya utulivu 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas alitoa mwito wa mazungumzo ili kuepuka janga kwenye kanda hiyo kufuatia mazungumzo baina ya Ugiriki na Uturuki.

türkischer Bohrschiff Yavuz
Picha: Reuters/M. Sezer

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO,Jens Stoltenberg alitoa pia mwito wa kupunguza mvutano na kuweko mazungumzo.

Kwa miaka mingi Uturuki na Ugiriki zote zimekuwa washirika muhimu wa jumuiya ya NATO. ''Tunataka kutafuta njia ya kupata ufumbuzi wa hali ya Mediterania mashariki,'' alisisitiza Stoltenberg.

Ugiriki na Uturuki zinatofautia kuhusu mipaka kwenye eneo la majini ambalo linaaminika kuwa na utajiri wa mafuta. Tayari mzozo huo ulisababisha mapigano baina ya manowari ya Uturuki na meli ya Ugiriki. Nchi zote mbili ziliendesha mazoezi ya kijeshi kwenye eneo hilo.