1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan apuuza vikwazo, aapa kuendeleza operesheni Syria

Daniel Gakuba
16 Oktoba 2019

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake itapuuza miito ya kuitaka isitishe operesheni za kijeshi kaskazini mwa Syria na kuongeza kuwa Uturuki haikoseshwi usingizi na vikwazo vipya ilivyowekewa na Marekani.

https://p.dw.com/p/3RMdd
Türkische Militäroffensive in Nordsyrien | Luftangriff in Ras al-Ain
Moshi ukifuka mjini Ras al-Ain kaskazini mwa Syria, baada ya shambulizi la ndege za UturukiPicha: AFP/D. Souleiman

Rais Erdogan ameeleza msimamo huo wa kukaidi miito ya jumuiya ya kimataifa, akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege yake, akirudi nyumbani kutoka Azerbaijan. Amesema jeshi la Uturuki kamwe halitasimamisha operesheni dhidi ya Wakurdi, hadi pale watakapokuwa wametimiza malengo yao, ambayo ni kuweka ukanda salama ndani ya mpaka waSyria, kuzuia mashambulizi ya Wakurdi ambao Uturuki inawaita magaidi.

Akizungumzia vikwazo vipya vya kiuchumi ambavyo Marekani iliiwekea Uturuki mwanzoni mwa juma hili, Rais Erdogan amesema vikwanzo hivyo vinalenga kuishinikiza serikali yake, ila akavipuuza akisema havimtii wasiwasi wowote.

Türkei PK Erdogan Syrien Invasion
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anasema hakoseshwi usingizi na vikwazo vya MarekaniPicha: Presidential Press Office

Rais huyo wa Uturuki alikiri kuwa mwanajeshi wa nchi yake aliuawa katika shambulizi lililofanywa na vikosi vya serikali ya Syria, vilivyowasili katika mji wa Manbij, ambao siku chache zilizopita ulidhibitiwa kwa pamoja na vikosi vya Marekani na vya Uturuki.

Jeshi la Syria lafurahiwa na wakazi wa Manbij

Jeshi la Syria liliingia katika mji huo baada ya makubaliano na kikundi cha Wakurdi kiitwacho Syrian Democratic Forces, SDF, baada ya Marekani kukitupa mkono kikundi hicho na kuwaondoa wanajeshi wake, hatua iliyofuatiwa na kuingia kwa Uturuki kaskazini mwa Syria. Baadhi ya wakazi wa Manbij wamefurahia kurejea kwa mji wao mikononi mwa serikali.

Russische und syrische Nationalflaggen auf Militärfahrzeugen in der Nähe von ManbijRussische und syrische Nationalflaggen auf Militärfahrzeugen in der Nähe von Manbij
Magari ya jeshi la Urusi yakiingia mjini Manbij. Urusi ni mshirika mkuu wa serikali ya mjini DamascusPicha: Reuters/O. Sanadiki

''Tulikuwa na hofu kwamba Uturuki ingevamia mji wa Manbij, lakini kuwepo kwa jeshi la Syria, kutaizuia Uturuki kufanya hivyo. Tunajisikia vyema na wenye amani.'' Alisema mmoja wao, na mwingine akaongeza, ''Kwa miaka minane tumekuwa tumetengwa na nchi yetu, lakini leo tumerejea. Tulikuwa tukiogopa kila upande, na mnamo miaka hiyo minane, tumeona watu wa kila aina.''

Heka heka za kidiplomasia

Shirika la habari la Urusi, Interfax limenukuu taarifa ya wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, iliyosema kuwa hivi sasa jeshi la serikali ya Syria linadhibiti eneo lenye ukubwa wa km 1000 za mraba kuzunguka mji wa Manbij, ikiwemo kambi ya jeshi ya Tabqa.

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence na Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo wanatarajiwa kuwasili nchini Uturuki hii leo kwa mashauriano, wakati ikulu ya Urusi ikithibitisha muda mfupi uliopita, kuwa Rais Erdogan wa Uturuki amekubali mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kufanya ziara ya kikazi mjini Moscow siku chache zijazo.

Putin na Erdogan wanaarifiwa kuafikiana juu ya umuhimu wa kuepusha makabiliano kati ya vikosi vya Uturuki na vile vya serikali ya Syria.

afpe, rtre