1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan atishia kuwafungulia wahamiaji mipaka kuingia EU

25 Novemba 2016

Ankara imekasirishwa na bunge la Umoja wa Ulaya kwa kuunga mkono usitishwaji  wa mazungumzo kuhusu uanachama wake. Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel asema vitisho kama hivyo havina faida

https://p.dw.com/p/2TGSt
Türkei Rede Erdogan bei der Sitzung der Parlamentarischen Versammlung der NATO in Istanbul
Picha: Reuters/M. Sezer

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametishia kuwa huenda akafungua mpaka wa nchi yake ili kuwaruhusu wahamiaji kufika katika mataifa ya Umoja wa Ulaya. Hatua hiyo inaweza kuvunjilia mbali makubaliano yaliyoafikiwa na ambayo yamesaidia kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Kitisho cha Erdogan kinajiri siku moja tu baada ya Ankara kukasirishwa na bunge la Umoja wa Ulaya kwa kuunga mkono usitishwaji  wa mazungumzo na Uturuki, kutokana na ukandamizaji wake ambao umeshuhudiwa tangu jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa ya Julai 15.

Erdogan amesema Umoja wa Ulaya ulililia usaidizi kutoka kwake mwaka 2015 wakati makumi ya maelfu ya wahamiaji walifika katika kivuko kilichoko kati ya Uturuki na Bulgaria wakitaka waruhusiwe kuingia Ulaya. Erdogan amewalaumu viongozi wa EU akisema, nchi yake inapowashughulikia wahamiaji milioni 2.7 kutoka Syria na Iraq, wao hawajafanya lolote kutimiza ahadi zao, na kusema EU haijawasilisha yuro  6 walizoahidi kusaidia wahamiaji.

Bango la ukaribisho wa mji wa Kapikule
Bango la ukaribisho wa mji wa KapikulePicha: picture-alliance/dpa/C. Hoffmann

Msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya Margaritisa Schinas amesema tume hiyo haitajiingiza kwenye matamshi ya kudhania na kwamba wapo katika harakati ya kutimiza makubaliano.

Matamshi makali ya hivi punde yaliyotolewa na Erdogan dhidi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya, yamesababisha Ujerumani kutoa onyo la haraka. Msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Ulrike Demmer amesema mkataba huo ulikuwa wa manufaa kwa pande zote husika na hivyo basi vitisho kama hivyo havina faida.

Uturuki ilikubali kushika doria katika fukwe zake na mpaka wa ardhini, kwa mpango wa kubadilishana faida. Faida yao ni kuzingatiwa ombi lao la kutaka kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya ombi ambalo limekwama  kwa muda mrefu, pamoja na kutaka raia wake waruhusiwe kusafiri bila visa kuingia nchi za Ulaya.

Baadhi ya wahamiaji Ugiriki
Baadhi ya wahamiaji UgirikiPicha: Reuters/G. Moutafis

Mchakato huo  ulitarajiwa kukamilika mwezi Oktoba lakini hakuna hatua iliyofua dafu na zaidi ya hayo bunge la Umoja huo wa Ulaya limepitisha jana kusitisha mazungumzo kuhusu ombi hilo la Uturuki. Ankara inailaumu Brussels kwa kutotimiza ahadi za upande wao kwenye mkataba huo ulioafikiwa tarehe 18 mwezi Machi ilhali wao wameendelea kushika doria katika fuo zao na mipaka yao kuwazuia wahamiaji wanaotumia bahari Aegian kati ya yao na Ugiriki.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, wahamiaji 171000 pekee ndio wamefika Ugiriki mwaka huu, tofauti na mwaka jana ambapo wahamiaji 740,000 walivuka.Mamia ya wahamiaji pia wamezama maji wakivuka bahari Aegian kwa kutumia maboti yaliyochakaa.

Wadadisi wa kisasa wanasema suala la uanachama wa Umoja wa Ulaya linakumbwa na pandashuka kuu na matumaini finyu kufuatia mambo kadha wa kadha yanayotishia kuliporomosha.

Mwandishii: John Juma/AFPE/DPE

Mhariri:Yusuf Saumu