1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kuzuru Berlin polisi wengi wakishika doria

John Juma
17 Novemba 2023

Idadi kubwa ya polisi inatarajiwa kushika doria mjini Berlin, wakati wa ziara ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambapo anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

https://p.dw.com/p/4Z1vr
Erdogan aitembelea Ujerumani
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Kayhan Ozer/AA/picture alliance

Ziara ya Erdogan ina utata kutokana na kauli zake kuhusu Vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Kauli kadhaa za Erdogan zimekuwa zikizusha ghadhabu tangu mashambulizi ya kigaidi ya wanamgambo wa Hamas mnamo Oktoba 7 nchini Israel, ambayo yaliua watu wapatao 1,200, na baadaye mashambulizi ya Israel ya kulipiza kisasi ambayo hadi sasa yameua zaidi ya watu 11,000

Rais Erdogan kuizuru Ujerumani leo

Erdogan hulitaja Hamas kuwa “kundi la ukombozi" na hulaani oparesheni za kijeshi za Israeli kama uhalifu wa kivita, akiishutumu Israel kwa kile alichokiita "ugaidi unaofanywa na serikali."

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeliorodhesha Hamas kama kundi la kigaidi. Ujerumani, kwa upande mwingine, husema usalama wa Israel ni “jukumu lake la kiserikali."

Maandamano kadhaa yameandaliwa Ujerumani wakati wa ziara hiyo itakayodumu kwa muda wa saa chache tu.

Kansela Scholz anamchukulia Erdogan kama mshirika muhimu wa mazungumzo kuhusu masuala kama vile kudhibiti uhamiaji kwenda Ulaya.