1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ziarani Ujerumani

Angela Mdungu
17 Novemba 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kuwasili mjini Berlin leo Ijumaa katika ziara fupi wakati nchi hizo mbili zikiwa na misimamo tofauti kuhusu vita kati ya Israel na Hamas.

https://p.dw.com/p/4Z1W9
Picha kutoka maktaba  Erdogan kuizuru Ujerumani
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Kayhan Ozer/AA/picture alliance

Ziara ya Erdogan inafuatia mwaliko uliotolewa na Kansela Olaf Scholz mwezi Mei baada ya rais huyo wa Uturuki kushinda uchaguzi kwa mara nyingine. 

Wakati wa ziara yake fupi Ujerumani Rais Recep Tayyip Erdogan atakutana na Kansela Olaf Scholz pamoja na rais Frank Walter Steinmeier.

Soma zaidi: Rais Erdogan kuzuru Ujerumani katikati mwa tofauti kuhusu Israel

Uturuki inachukuliwa kuwa mshirika tata lakini muhimu wa Ujerumani ambayo ina zaidi ya watu milioni 3 wenye asili ya Uturuki. Licha ya kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mivutano kuhusu masuala kadhaa Nchi hiyo pia ni mshirika muhimu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO katika juhudi za kudhibiti wahamiaji wanaoingia Ulaya.

Maelfu ya maafisa wa polisi wasambazwa Berlin kuimarisha Usalama

Maafisa wa polisi wasiopungua 1,500 wanatarajiwa kuimarisha ulinzi wakati wa ziara hiyo ya leo katika makazi rasmi ya Rais wa Ujerumani na kwenye Ubalozi wa Uturuki. Safari yake hiyo Erdogan imegubikwa na mpasuko kuhusu misimamo ya nchi hizo mbili juu ya mzozo wa Israel na kundi la Hamas baada ya mashambulizi yaliofanywa Oktoba 7 ndani ya Israel na kundi hilo.  

Kansela Scholz na Rais Erdogan katika mkutano wa NATO
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Soma zaidi: Erdogan ahutubia maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Hayo yanajiri wakati ndani ya Ujerumani, ndugu wa mateka 11 wanaoshikilikiliwa na kundi la Hamas wamezungumza wakiwashinikiza viongozi wa nchi hiyo kutokwepa kulizungumzia hilo wakati wa ziara ya Erdogan. Maandamano kadhaa yamepangwa kufanyika wakati wa ziara yake itakayodumu kwa saa chache. Itakumbukwa kuwa Rais Erdogan  amekuwa akilielezea kundi la Hamas kama kundi la ukombozi na amelaani hatua zilizochukuliwa na jeshi la Israel kuwa uhalifu wa kivita akiituhumu nchi hiyo kwa ugaidi. 

Jumatano wiki hii, Kansela Olaf Scholz aliliambia bunge kuwa mazungumzo yake na rais wa huyo wa Uturuki yatajumuisha mitizamo tofauti na kuongeza kuwa ni muhimu kuweka mambo bayana na wanachokisimamia.