1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres awasilisha ajenda mpya ya amani ya ulimwengu

Sylvia Mwehozi
21 Julai 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasilisha muhtasari wa sera inayohusu Ajenda mpya ya amani ambayo imebainisha mkakati wa juhudi za kimataifa za amani na usalama kwa kuzingatia sheria ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/4UDY4
Antonio Guterres | Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António GuterresPicha: Yuki Iwamura/AFP/Getty Images

Akihutubia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa siku ya Alhamis, Guterres amesema kwamba ulimwengu upo katika "Enzi mpya" na kwamba kipindi cha baada ya Vita Baridi kimemalizika na ulimwengu unaelekea kwenye mpangilio mpya wa kimataifa unaohusisha nchi kadhaa kuwa na nguvu zaidi. 

Soma kuhusu sera hiyo: Mkuu wa Umoja wa Mataifa apendekeza mabadiliko ya kisera

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres, "enzi hizi mpya tayari zimetawaliwa na kiwango kikubwa cha mivutano ya siasa za kikanda na ushindani mkubwa wa mataifa yaliyo na nguvu kwa miongo" na kwamba "nchi nyingi wanachama zinaendelea kushikwa na wasiwasi ikiwa mfumo huo wa pande nyingi unazinufaisha". Aidha mkuu huyo ameongeza kwamba "ukiukaji wa sheria ya kimataifa umekuwa jambo la kawaida".

"Wakati huo huo, ulimwengu unakabiliwa na vitisho vipya na vile vinavyoendelea, vinavyohitaji hatua za haraka na za pamoja. Migogoro imekuwa migumu zaidi, yenye kuua na migumu kusuluhishwa. Mwaka jana ulishuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyohusiana na migogoro kwa takribani miongo mitatu. Wasiwasi kuhusu uwezekano wa vita vya nyuklia umeibuka tena," alisema Guterres.

New York | António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipokuwa akihutubia Mkutano mkuu wa UN mwezi Machi 2023.Picha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua News Agency/picture alliance

Guterres ameonya kuwa migawanyiko hii inadhoofisha msingi wa Umoja wa Mataifa wa nchi zote kushirikiana kutatua changamoto za kimataifa. Katika hotuba yake, Guterres pia aligusia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kwamba umefanya mambo kuwa magumu zaidi katika kuelezea changamoto hizo. Bila ya kuitaja Urusi, lakini alikosoa kwa uwazi akisema kwamba kama kila nchi ingetimiza wajibu wake, chini ya sheria za Umoja wa Mataifa, za kuheshimu uhuru na uadilifu wa mataifa yote, basi "haki ya amani ingelindwa".

Soma pia: Viongozi waungane kumaliza changamoto za demokrasia na usalama, Afrika.

Moja ya maeneo muhimu ambayo ajenda hii mpya inayopendekeza imekuwa dhahiri ni katika operesheni za kulinda amani, haswa kufuatia kura ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mwezi Juni ya kumaliza mara moja ujumbe wake wa kulinda amani nchini Mali. Hatua hizo zilifikiwa baada ya serikali ya kijeshi ya Mali kutaka ujumbe huo kuondoka na kuwaleta wapiganaji mamluki wa kundi la Wagner la nchini Urusi ili kupambana na waasi wenye itikadi kali.

Guterres amewaeleza wanadiplomasia kwamba wakati walinzi wa kulinda amani wameokoa mamilioni ya maisha, "migogoro ya muda mrefu ambayo haijapatiwa ufumbuzi, ya ndani, kikanda na kimataifa imefichua ukomo wake" akiongeza kuwa "opresheni za kulinda amani haziwezi kufanikiwa ikiwa hakuna amani ya kudumu".Lavrov ziarani Mali

Ajenda ya awali ya amani iliwasilishwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Boutros Boutros-Ghali mwaka 1992 kufuatia kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti na mwisho wa Vita Baridi na Marekani. Ilikaribisha mwisho wa "uadui na kutoaminiana" kati ya mataifa makubwa na kuelezea jinsi Umoja wa Mataifa unavyoweza kuongeza majukumu yake katika diplomasia ya kuzuia, kulinda na kujenga amani.

Vyanzo: EBU/AP/AFP