1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuendelea leo jioni.

Mtullya, Abdu Said12 Agosti 2008

Shirika la kutetea haki za binadamu duniani Human Rights Watch lataka umwagaji damu ukomeshwe nchini Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/EvW3
Rais Robert Mugabe atakiwa akomeshe umwagaji damu nchini Zimbabwe.Picha: AP

Wakati mazungumzo  juu  ya  kutatua mgororo wa   kisiasa nchini  Zimbabwe yanatarajiwa kuendelea  leo jioni, shirika la kutetea  haki za binadamu  duniani, Human Rights Watch limetoa mwito kwa viongozi  wa kusini mwa Afrika juu ya kuishinikiza serikali  ya   Mugabe ili ikomeshe  umwagaji  damu  unaondelea nchini  Zimbabwe.


Shirika  la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch  limetoa mwito huo leo  katika ripoti yake juu  ya kuandamwa wapinzani na wanaharakati wa  kisiasa nchini Zimbabwe.

Wakati  mazungumzo juu ya kugawana mamlaka  yanatarajiwa kuendelea jioni ya leo baina ya  wawakilishi wa serikali ya Mugabe na wa chama cha upinzani MDC, shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao  mjini New York limekilaumu  chama kinachotawala nchini Zimbabwe  Zanu PF na wafuasi wake kwa kuendeleza mauji, kuwashumbulia   na kuwatia ndani wabunge wa  chama  cha upinzani  na wanaharakati wengine wa kisiasa.

Kutokana na madai hayo asasi hiyo ya kutetea haki   za binadamu inawataka viongozi wa nchi za jumuiya  ya maendeleo ya kusini mwa  Afrika SADC wawe  na msimamo thabiti kwenye mkutano wao  wa jumamosi ijayo katika kupinga  kukiukwa haki  za binadamu nchini Zimbabwe.

Shirika la Human Rights Watch limesema jumuiya ya   maendeleo ya kusini mwa  Afrika SADC inapaswa kuhakikisha  kwamba  polisi ya Zimbabwe  inavunja   haraka, kambi na vituo vya  mateso  vyote vilivyopo nchini kote.

Wakati  huo huo  msuluhishi katika mgororo  wa   Zimbabwe rais Thabo Mbeki  wa  Afrika Kusini  anaetarajiwa kuchukua  uenyekiti wa  jumuiya  ya SADC kwenye mkutano  wa  jumamosi amekuwa anajaribu  kuwashawishi  rais Robert Mugabe na   viongozi  wa upinzani wafikie makubaliano juu ya mapendekezo ya kugawana  mamlaka ili kuutatua  mgogoro wa nchi yao.

Mazungumzo juu ya mgororo huo yanatarajiwa kuendelea leo jioni.Lakini wawakilishi wa chama cha Mugabe Zanu PF na wa chama cha  upinzani MDC bado wanatofautiana  juu ya ugawanaji wa mamlaka katika serikali mpya. Mafanikio ya mazungumzo hayo yatatoa mchango mkubwa katika kuweka mazingira  ya kuujenga upya  uchumi wa  Zimbabwe.

Lakini  mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za   binadamu la  HRW, kanda ya Afrika Georgette  Gagnon amedai kuwa chama cha  Zanu PF   kinaendelea  na matendo ya umwagaji damu na hivyo kinahujumu uadilifu wake.

Mkurúgenzi huyo amemtaka rais Mbeki aweke mkazo katika kuleta suluhisho  la kudumu badala  ya kutafuta  suluhisho la muda  tu. Lakini  rais  Mbeki  amesema kuchukua  msimamo mkali  dhidi ya rais Mugabe kutafanya mvutano  uwe mkubwa  zaidi  na kuweza  kuathiri juhudi  za  kuleta  suluhisho.