1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna maafikiano kuihusu Syria huku Papa akitangaza siku ya maombi kote duniani

7 Septemba 2013

Mkutano wa viongozi wa nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20 umekamilika jana(06.09.2013) huku viongozi hao wakiwa wametofautiana kuhusu mzozo wa Syria na baba mtakatifu Francis akitoa wito wa maombi ya amani

https://p.dw.com/p/19dOT
Picha: Reuters

Mkutano wa viongozi wa nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, G20 umekamilika jana(06.09.2013) huku viongozi hao wakiwa wametofautiana kuhusu mzozo wa Syria.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alidhihirisha wazi msimamo wake wa kupinga kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Syria kwa kusema kufanya hivyo kutayumbisha kanda hiyo.

Rais wa Marekani Barack Obama kwa upande wake amesema ni muhimu hatua hiyo ya kijeshi kuchukuliwa kuiadhibu Syria kwa matumizi ya silaha za kemikali.

Obama ameelezea wasiwasi wake kutokana na kutokuwa kwa umoja kuhusu jinsi ya kulishughulikia suala hilo kutoka jamii ya kimataifa.Putin anawashutumu waasi nchini Syria kwa matumizi hayo ya sumu akidai waliitumia wakitumai hilo litachochea nchi ambazo zinawaunga mkono kuchukua hatua dhidi ya Assad.

Nchi zagawanyika kuhusu Syria

India, Afrika kusini na China ni miongoni mwa nchi zinazopinga hatua za kijeshi dhidi ya Syria.Taarifa ya pamoja kutoka Marekani na nchi nyingine kumi zimetaka hatua kali kuchukuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters

Syria ilikuwa pia ajenda kuu katika mkutano wa mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro uliofanyika jana mjini Vilnius nchini Lithuania.

Ujerumani,Sweden,Italia,Ugiriki na Uhispania zinapinga hatua za kijeshi dhidi ya Syria bila idhini ya umoja wa Mataifa. Mawaziri wa ulinzi wa umoja wa Ulaya pia walikutana katika mji huo mkuu wa Lithuania kwa kikao kisicho rasmi na kukubaliana kuwa ushahidi unaashiria kuwa utawala wa rais Bashar al Assad ndio uliotumia silaha za kemikali katika vita vya Syria.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton anatarajiwa kutoa tangazo rasmi kuhusu msimamo wa umoja huo kuihusu Syria leo asubuhi baada ya mawaziri hao kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Kanisa katoliki limetoa wito kwa waumini wake,wa madhehebu mengine na dini nyingine kutenga leo kuwa siku ya kimataifa ya kufunga na kuomba kwa ajili ya amani Syria huku viongozi wa dunia wakitofautina kuhusu mzozo unaokumba nchi hiyo.

Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis atoa wito wa maombi juu ya Syria
Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis atoa wito wa maombi juu ya SyriaPicha: Reuters

Kiongozi wa kanisa katoliki baba matakatifu Francis anatarajiwa kuendesha misa katika ukumbi wa St Peters katika makao makuu ya kanisa katoliki Vatican leo Jumamosi ili kuiombea Syria na kuepusha hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Ni kufunga na kuomba kwa ajili ya amani Syria

Papa Francis amewataka wakristo na waumini wa dini nyingine kote ulimwenguni kujitokeza leo kufunga na kuomba ili kupatikane amani nchini Syria ambako kumekuwa na vita kwa zaidi ya miaka miwili sasa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki moja na mamilioni wengine kuachwa bila makaazi.

Kiongozi wa dhehebu la kisunni nchini Syria Mufti Ahmad Badreddin Hassoun amewataka raia wa Syria kujiunga na maombi hayo ya kuliombea taifa lao na kiongozi pia wa dhehebu la kiorthodoksi duniani Constantinople Bartholomew 1 amesema anaunga mkono wito huo wa papa.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Daniel Gakuba