1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Zimbabwe inatisha

Oumilkher Hamidou25 Novemba 2008

Tume ya wazee yaonya dhidi ya kusambaratika Zimbabwe

https://p.dw.com/p/G1bX
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP


Tume ya kiutu inayoongozwa na rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter imetoa mwito wa kufumbuliwa haraka mzozo wa Zimbabwe.Mwito huo umetolewa jana mjini Cape Town nchini Afrika kusini ambapo wawakilishi wa serikali na wale wa upande wa upinzani wanatazamiwa kukutana hii leo kujaribu kwa mara nyengine tena kuupatia ufumbuzi mzozo huo.


Tume hiyo ya wazee iliyoundwa na rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson Mandela,imeonya dhidi ya kitisho cha kuangamia Zimbabwe .Baada ya mazungumzo pamoja na upande wa upinzani,mashirika ya huduma za jamii,mashirika ya Umoja wa mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kiutu,wajumbe wa tume hiyo inayowaleta pamoja rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter,katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan na mke wa rais mstaafu wa Afrika kusini bibi Graca Machel,wamesema hali ya mambo nchini Zimbabwe inatisha zaidi kuliko ilivyokua ikifikiriwa.Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter anazungumzia juu ya hali yenyewe akisema:


"Mshahara wa waalimu kwa mwezi ni dola moja ya kimarekani.Asili mia 20 tuu ya watoto ndio wanaomudu kwenda shule.Mwaka jana walifikia asili mia 85.Na anaekwenda shule,pengine anakuta hakuna mwalimu kwasababu mwalimu hana pesa za kulipia nauli.Vyuo vikuu vyote vya serikali vimefungwa."


Na mfumo wa afya pia umevurugika.Hospitali kuu nne za nchi hiyo zimefungwa-mbili kati ya hospitali hizo ziko katika mji mkuu Harare.Watu 6300 wanasemekana wameambukizwa maradhi ya kipindu pindu yaliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 300 hadi sasa.Kinachotisha zaidi lakini ni njaa.Idadi ya watu wanaotegemea misaada ya chakula imeongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja toka watu milioni mbili na laki sita na kufikia watu milioni nne na laki tisaa- january mwakani watafikia watu milioni tano na laki moja-kwa maneno mwengine nusu ya wakaazi wa Zimbabwe.Ili kuepukana na balaa kubwa zaidi la njaa,panahitajika msaada wa dala milioni 140 kwa mwaka huu na mwakani dala milioni 550.Rais wa zamani wa Marekani anaendelea kusema:


"Yote haya yanaonyesha kwamba hali inatisha zaidi kuliko namna tuilivyofikiria.Ni wazi kabisa kwamba ukosefu wa serekali madhubuti ndio chanzo kikuu cha mzozo wa Zimbabwe."


Jimmy Carter,Kofi Annan na Graca Machel wanaituhumu jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC kutofanya vya kutosha dhidi ya mzozo wa Zimbabwe.Wamemlaumu sana Robert Mugabe wanaesema tunanukuu:"sio tuu amewakatalia ruhusa ya kuingia humo nchini, lakini anaonyesha pia kuupuuza mzozo wa Zimbabwe.Hata hivyo wajumbe hao watatu wamezitolea mwito pande zote mbili, rais Robert Mugabe na upande wa upinzani wakubali kurejea katika meza ya majadiliano kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Zimbabwe.