1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas na Fatah wakubaliana kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa

Abdu Said Mtullya28 Aprili 2011

Hamas na Fatah wakubaliana kuweka kando uhasama baina yao

https://p.dw.com/p/115Do
Rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas kushoto, na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa

Vyama hasimu vya Fatah na Hamas vimefikia mapatano ya kuunda serikali ya Umoja ya mpito.

Iwapo mapatano hayo yatatekelezwa,hiyo itakuwa hatua ya kwanza muhimu ya kuelekea katika kuundwa taifa huru la Wapalestina.

Kwa mujibu makubaliano yaliyofikiwa kutokana na upatanishi wa Misri, Hamas na Fatah wataunda serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa na kuitisha uchaguzi mnamo kipindi cha miezi minane ijayo.

Kiongozi wa ujumbe wa Fatah Azzam al Ahmad aliliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha uchaguzi wa Rais na wa Bunge .Bwana Ahmad pia ameeleza kuwa serikali hiyo itakuwa ya pande mbili huru.Amesema Wapalestina sasa wanayo silaha madhubuti dhidi ya kukandamizwa, akiwa na maana ya umoja wa wapalestina.

Wapalestina wakifurahia maamuzi mapya ya Hamas na Fatah kuunda serikali ya pamoja
Wapalestina wakifurahia maamuzi mapya ya Hamas na Fatah kuunda serikali ya pamojaPicha: ap

Kiongozi wa ujumbe wa chama cha Hamas bwana Mahmud Zahar aliliambia shirika la televisheni la Aljazeera kuwa serikali itakayoundwa itatokana na wanasiasa watakaochaguliwa kutoka pande zote mbili.

Akizungumza mara ya baada kutangazwa habari juu ya makubaliano hayo kiongozi mwengine wa Hamas Abu Marzouk alisema kuwa habari hizo nzuri zimekimaliza kipindi cha maumivu katika historia ya Wapalestina.

Nchini Israel habari juu ya mapatano ya Hamas na Fatah zimepokelewa kwa ghadhabu.Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu amemwonya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas kwa kusema kwamba kiongozi huyo wa Wapalestina sasa hana budi achague baina ya kudumisha amani na Hamas au na Israel.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Netanyahu amemwambia Mahmoud Abbas kuwa haitawezekana kudumisha amani na pande zote mbili. Naye waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman amesema kuwa mapatano yaliyofikiwa baina ya Hamas na Fatah ya kuunda serikali yamevuka mpaka wa hatari.

Waziri Lieberman amekishutumu kipengele cha makubaliano kinachotaka wafungwa wa Hamas waachiwe na amedai kwamba Hamas itauteka Ukingo wa Magharibi ambao kwa sasa upo chini ya uongozi wa chama cha Fatah. Waziri huyo ameitaka jumuiya ya kimataifa isisitize kwa serikali yoyote mpya ya wapalestina itakayoundwa , iyatekeleze masharti matatu ikiwa pamoja na kuitambua haki ya kuendelea kuwapo taifa la Israel, kuachana na matendo ya kutumia nguvu na kuyakubali mapatano ya amani yaliyofikiwa katika siku za nyuma.

Misri itawaalika mjini Cairo viongozi wa Hamas na Fatah ili kuyatia saini makubaliano yaliyofikiwa.Kwa mujibu wa mapatano hayo uchaguzi wa Rais na wa Bunge utafanyika wakati mmoja katika kipindi cha miezi minane ijayo.

Hamas na Fatah wamekuwa mahasimu tokea mwishoni mwa miaka ya 90. Uhusiano ulizidi kuwa mbaya baina yao baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2006 ambapo chama cha Hamas kilikishinda chama cha Fatah na kufanikiwa kupata zaidi ya nusu ya viti vya bunge.

Hamas iliwatimua Fatah kutoka Ukanda wa Gaza baada ya mapambano, na hivyo kuwagawa Wapalestina katika pande mbili Hamas katikaUkanda wa Gaza na Fatah kwenye Ukingo wa Magharibi.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFP/ZA/

Mhariri/_ Josephat Charo