1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisia kuhusu hotuba ya Rais Samia katika Baraza Kuu la UN

George Njogopa24 Septemba 2021

Kumekuwa na maoni mchanganyiko nchini Tanzania juu ya namna Rais Samia Suluhu Hassan alivyowasilisha hotuba yake ya kwanza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huku wengi wakionekana kuvutiwa na kupongeza kuhusiana na masuala aliyogusia.

https://p.dw.com/p/40nRU

Mambo kama Tanzania kuendelea kuwa mshirika wa karibu katika siasa za kimataifa, kusaka nguvu ya pamoja kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona, ni baadhi ya mambo ambayo yamempa alamu kiongozi huyo wa wamu ya sita. Hata hivyo, baadhi wanaonekana kusita kutoa heko ya moja kwa moja hasa pale inapohusika na suala la ukuzaji demokarasia nchini humo.

Rais Samia anaonekana kuwagusa wengi katika hotuba yake hiyo iliyoitoa jana usiku mbele ya halaiki ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hasa kutokana na namna alivyogusia masuala muhimu yanayoendelea kigubika dunia na kwa namna alivyohimiza haja ya kukusanya nguvu ya pamoja katika kuyatafutia majawabu masuala hayo.

Hakuishia tu katika kuitaka dunia kutoyaacha nyuma mataifa yanayoendelea katika vita ya kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona akisema maendeleo ya dunia yanaweza kujikuta yakirudi nyuma kwa kasi ya ajabu  iwapo kila nchi itajichukulia njia yake katika kulishughulikia janga hilo.

Tathmini ya hotuba ya Rais Samia katika Baraza Kuu la UN

Wengi wanampa heko kwa namna alivyopangilia hotuba yake na kwa mfano mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Gwatumi Mwakatobe anasema Rais Samia ameanza na mguu sahihi ndani ya chombo hicho cha kimataifa.

Rais Samia aligusia pia masuala kama hatua anazochukua katika kumwezesha mwanamke kupanda katika ngazi mbalimbali za uongozi na hatimaye kufikia shabaha ya uwiano sawa na mwanamme. Kama hiyo haitoshi aligusia pia suala la demokrasia alikosema inashamiri.

Kauli yake hiyo imeibua ukosoaji kutoka kwa makundi ya baadhi ya wasomi na wanasiasa wanaona kwamba Tanzania bado inaendelea kuburuta miguu pale inapozungumziwa demokrasia ya ukweli.

Sammy Ruhuza ambaye  amewahi kuwa mwanasiasa wa chama cha upinzani na mchambuzi wa masuala hayo hayo ya kisiasa, anaona kuwa kama kutoa alama kuhusu kiwango cha demokrasia  alama ambayo Tanzania inayoweza kupata ni ile ya chini kutokana na mazingira yanayoendelea kushuhudiwa wakati huu.

Rais wa tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 23, 2021.
Rais wa tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 23, 2021.Picha: Timothy A. Clary/AP Photo/picture alliance

Hoja kubwa inayotolewa na wale wanaofuatilia hali ya kisiasa nchini Tanzania ni ile inayohusu kubinywa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uhuru ikiwamo kupigwa marufuku kufanya mikutano ya hadhara na hata ile ya ndani iliyoruhisiwa katika siku za hivi karibuni bado inaingiliwa na jeshi la polisi.

Hata hivyo, mkuu wa jeshi la polisi IGP, Simon Sirro ambaye jeshi lake limefanya majadiliano ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa anasema hali hiyo inatokana na mkanganyiko kwenye sheria.

Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imeweka shabaha ya kukutana na makundi mbalimbali katika kile inachosema ni jitihada za kumaliza mvutano kati ya vyama vya siasa na jeshi la polisi.