1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu ya mgawanyiko katika mkutano wa kilele wa G20 India

John Juma
8 Septemba 2023

Viongozi wa mataifa 20 tajiri zaidi ulimwenguni wanaelekea India kwa mkutano wa kilele wikendi hii.

https://p.dw.com/p/4W6m6
Indien I G20 in Neu Delhi
Picha: Channi Anand/AP/dpa/picture alliance

Viongozi hao wanakutana katika mwaka wenye joto zaidi katika historia ya binadamu, lakini matumaini ni madogo kwamba wataweza kukubaliana kuhusu hatua kabambe za kukabili mgogoro huo.

Mivutano ya kisiasa ya kikanda ambayo imesababisha rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa China Xi Jinping kutohudhuria mkutano huo, inamaanisha huenda viongozi hao wasiweze kupata muafaka wa pamoja na hata ahadi za kushughulikia tabianchi.

Masuala matatu muhimu yatakayojadiliwa kwenye  mkutano wa New Delhi  ni msukumo wa kuongeza nishati mbadala duniani mara tatu ifikapo mwaka 2023; kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku, na ufadhili kwa nchi maskini kutumia nishati salama.

Hapo jana Alhamisi, shirika la Amnesty International lilitahadharisha kuhusu kile lilichokiita "uwezekano wa janga la kushindwa” kwa mataifa hayo ambayo yanachangia asilimia 80 ya utoaji wa hewa ukaa kote duniani.