1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya Ebola yatishia kuenea Afrika Magharibi

Oumilkher Hamidou4 Aprili 2014

Nchi kadhaa za Afrika magharibi zimepania kuipiga vita homa hatari ya Ebola iliyoangamiza maisha ya zaidi ya watu 80 nchini Guinea,siku moja tu baada ya homa hiyo kuripotiwa Mali,baada ya Liberia na Sierra Leone.

https://p.dw.com/p/1BcFY
Wauguzi katika hospitali moja ya GuineaPicha: picture alliance/AP Photo

Mali nchi inayopakana na Guine imesema jana usiku,kadhia tatu za homa ya Ebola zimegunduliwa nchini humo na walioambukizwa kuwekwa karantini.

"Watu hao watatu hali yao hivi sasa ni nzuri,hakuna tena dalili ya kuvuja damu-mojawapo ya ishara za homa ya Ebola" amesema waziri wa afya na usafi wa jamii Ousmane Koné.Kwa mujibu wa Dr. Omar Sangaré,wa idara ya afya watu hao wote watatu ni raia wa Mali waliokuwa wakifanya kazi katika eneo la mpakani kati ya Mali na Guine.

Serikali ya Mali imewaonya raia wasifike katika maeneo ya maambukizi.

Nchi iliyoathirika zaidi ni Guine ya Conacry ambako homa hiyo inayosababisha watu kuvuja damu imeshaangamiza maisha ya watu 86 toka jumla ya watu 137 walioambukizwa tangu january mwaka huu-wengi wao ni wa kutoka eneo la kusini-kwa mujibu wa ripoti ya serikali.

Ishara za matumaini mema

Kadhia 45 kati ya hizo zimethibitishwa kuwa ni za homa ya Ebola,maradhi hatari yanayoambukiza na ambayo hadi wakati huu hayana tiba wala chanjo."Lakini wagonjwa wawili waliokuwa wamewekwa karantini wamethibitishwa wamepona mjini Conacry"-serikali imesema.

WHO Ebola Afrika Schutzanzüge
Watumishi wa shirika la Afya la Umoja wa MataifaPicha: Isaac Kasamani/AFP/Getty Images

Matumaini finyu yamechomoza katika wakati ambapo shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka ,linaloendesha shughuli zake nchini Guine linazungumzia juu ya "mambukizi yasiokuwa na mfano".

Liberia inazungumzia kisa cha msasi mmoja ambae hakuwa na maingiliano na mtu yeyote aliyeambukizwa homa ya Ebola na wala hakuwahi kwenda Guinea.Liberia imewataka wakaazi wake wasinunue nyama yoyote inayotokea vijijini.Kadhia 14 za homa ya Ebola zimeripotiwa nchini Liberia-sabaa ya wagonjwa hao wameshakufa.

Nchi zinazopakana na Guinea zimetuma wataalam wa afya katika maeneo ya mpakani.Katika nchi ambako maradhi hayo ya kuambukiza yameshaingia maafisa wa serikali wanawapa mwongozo wa kuishi wananchi ili kuepukana na balaa la kuenea maradhi hayo.

Wataalam wa kimataifa wanawajibika

Wataalamu tangu wa ndani mpaka wa nje ya bara la Afrika wameingia mbioni kupambana na maradhi hayo hatari."Ugonjwa huu wa kuambukiza ni hatari kwasababu bado haujadhibitiwa na walioambukizwa wameenea sehemu tofauti" amesema tabibu mmoja wa kifaransa Sylvain Baize anaeongoza kituo cha utafiti wa homa zinazosababisha watu kuvuja damu mjini Lyon kusini mwa Ufaransa.

Hochsicherheitslabor
Maabara maalum ya kuchunguza vrusi vya homa ya EbolaPicha: picture-alliance/dpa

"Nimeingiwa na wasi wasi kwasababu haijulikani bado viruusi vya maradhi ya Ebola vimefika vipi katika eneo la Afrika magharibi na hakuna ajuaye watu wangapi hasa wameambukizwa" amesema kwa upande wake Thomas Geisbert,ambae ni mtaalam wa homa zinazopelekea watu kuvuja damu ,anaefanya kazi na kituo cha utafiti cha chuo kikuu cha Texas nchini Marekani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir /AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman