1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroEthiopia

HRW: Umoja wa Mataifa uchunguze mauaji ya jeshi la Ethiopia

5 Aprili 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Mataifa uchunguze uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Ethiopia katika eneo la Amhara, ambalo limekuwa likizongwa na mizozo.

https://p.dw.com/p/4eRqR
Eneo la mkoa wa Amhara
Eneo la mkoa wa Amhara Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Tume ya Haki za binadamu ya Ethiopia ilikadiria mwezi Februari kwamba watu wapatao 45 waliuliwa Januari 29 na vikosi vya serikali katika mji wa Merawi kufuatia mapigano na wapiganaji wa kundi la Fano. 

Shirika la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Afrika usitishe upelekaji wa vikosi vya serikali ya Ethiopia kwa tume za amani mpaka makamanda waliohusika na ukiukaji mkubwa wa haki wawajibishwe.

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika, Laetitia Badr, amesema kushindwa kwa serikali ya Ethiopia kuhakikisha uwajibikiaji wa maana kwa ukiukaji uliofanywa na vikosi vya serikali kuu na vya eneo hilo unachangia mzunguko wa machafuko na kufanya uhalifu bila kujali kuchukuliwa hatua kisheria.