1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF na kundi la G-20 zatoa nafuu kwa mataifa masikini

Admin.WagnerD16 Aprili 2020

Shirika la fedha la kimataifa, IMF limeamua kutoa mikopo ya dharura kwa nchi masikini pamoja na kusimamisha ulipaji wa riba za madeni kwa nchi hizo. Hatua hiyo imesisitizwa pia na nchi za kundi la G20. 

https://p.dw.com/p/3azWo
Kristalina Georgieva
Kristalina Georgieva, Mkurugenzi Mkuu wa IMFPicha: Reuters/R. Casilli

Nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi G20 zimekubaliana kusimamisha kwa muda ulipaji wa madeni kwa nchi masikini, chini ya mpango maalumu wa kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Nchi hizo masikini zimepewa muda wa kuanzia Mei mosi kusimamisha ulipaji wa riba hadi mwishoni mwa mwaka.

Rais wa Benki ya Dunia David Malpass pamoja na mkurugenzi washirika la fedha duniani IMF Kristalina Georgieva wamesema katika tamko lao la pamoja kwamba hatua hiyo muhimu sana itasaidia katika kuokoa maisha na njia za vipato kwa mamilioni ya watu waliomo katika hatari ya kukumbwa vibaya na athari zinazotokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Viongozi hao wa Benki ya dunia na shirika la IMF wameeleza kuwa wanatarajia mabenki ya biashara nayo pia yatachukua hatua kama hizo.

Japan Maas spricht bei G20-Treffen mit Cavusoglu
Picha: picture-alliance/dpa/E. Hoshiko

Kundi la G20 ambalo linazileta pamoja nchi zenye uchumi ulioendelea na zile zinazoinukia limesisitiza kuwa zitaweka tayari nyenzo zote kwa ajili ya kuzikabili athari zilizosababishwa na mlipuko wa maradhi na migogoro ya kiuchumi.

Wakati huo huo shirika la fedha duniani IMF limesema kuwa uchumi wa dunia utanywea kwa asilimia tatu mnamo mwaka huu na limesema hali inaweza kuwa mbaya zaidi kuliko ile iliyosababishwa na mgogoro wa kifedha ulioikumba dunia mwongo mmoja uliopita.

Nchi za Afrika kwa pamoja zimetoa wito wa kupatiwa msaada wa fedha kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

IMF imesema nchi za G 20 tayari zimeahidi kutoa kiasi cha dola trilioni 8 kusaidia juhudi za kupambana na janga la corona.

Vyanzo:/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga