1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ivanka kuzuru Berlin mwezi Aprili

27 Machi 2017

Mwanamitindo huyo aliyegeuka kuwa mshauri wa baba yake aliandika kuhusu ziara yake ya Berlin katika ukurasa wake wa Facebook usiku wa kuamkia Jumatatu. (27.03.2017)

https://p.dw.com/p/2a35X
USA Merkel und Trump suchen nach gemeinsamer Arbeitsebene | Merkel und Ivanka Trump
Picha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

Mtoto wa kike wa rais wa Marekani Donald Trump, Ivanka, amekubali mualiko wa kansela wa Ujeruamani, Angela Merkel, kuzuru Berlin mwezi ujao kuhudhuria mkutano wa kuwajengea uwezo wanawake. "Nataraji kushirikiana pamoja mjini Berlin mwezi ujao kuimarisha jukumu la wanawake katika uchumi na mustakabali wa nguvu kazi yetu W20."

Jukwaa la Mdahalo W20 litaandaliwa chini ya mwavuli wa mkutano wa kundi la mataifa yaliyostawi kiviwanda na yanayoinukia kwa kasi kiuchumi, G20, ambalo mwenyekiti wake ni Ujerumani. Hatua ya Merkel kumualika Ivanka kwa ajili ya mkutano huo wa wanawake huenda ikamsaidia kansela huyo kuhakikisha kwamba Donald Trump anachukua jukumu muhimu katika mkutano wa wakuu nchi na serikali wa kundi la G20 mwezi Julai mjini Hamburg, ambao anatarajiwa kuhudhuria, huku Merkel akiwa mwenyekiti.

Jukwaa la W20 linalowawakilisha wanawake kutoka sekta ya biashara, sayansi na jamii kwa ujumla, linatarajiwa kufanyika Berlin Aprili 25 na 26. Litatuwama juu ya ushiriki wa soko la ajira, pamoja na upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wanawake na njia za kuliziba pengo la kidigitali kati ya wanawake na wanaume.

Akijulikana kama "Msichana wa Kwanza" Ivanka Trump, analiona jukumu lake katika ikulu ya Marekani kama la kuusaidia utawala wa babake kutilia maanani masuala ya wanawake, hususan katika soko la ajira. Ziara ya Berlin itakuwa ya kwanza ya kimataifa ya Ivanka tangu baba yake alipoapishwa kama rais wa Marekani Januari 2017. Ivanka mwenye umri wa miaka 35 na ambaye ni mshauri anayeaminika zaidi na baba yake, alikutana na Merkel wakati kansela huyo alipoitembelea ikulu mapema mwezi huu.

Mwandishi:Josephat Charo/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu