1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji Luvanda ajitoa katika kesi ya CHADEMA

Amina Mjahid
6 Septemba 2021

Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi inayomkabili mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amejitoa kuendelea na kesi hiyo kutokana na upande wa washtakiwa kuonyesha hali ya wasiwasi

https://p.dw.com/p/3zz9l
Tansania | Freeman Mbowe
Picha: Amas Eric

Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, amesema anajiweka kando kuendelea kuendesha kesi hiyo muda mfupi baada ya Mbowe kutilia mashaka akisema hana imani na jaji huyo aliyetupilia mbali mapingamizi mawili kati ya matatu yaliyowekwa na mshtakiwa.

Kutokana na hatua hiyo, sasa Mbowe ataendelea kusalia rumande akisubiri shauri lake kupangiwa jaji mwingine na bado haijafahamika ni lini ofisi ya msajili wa mahakama itafanya kazi hiyo.

Kulingana na wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala washtakiwa walifikia hatua ya kuonyesha kutokuwa na imani na Jaji Luvunda, baada ya jaji huyo licha ya kuafiki pingamizi lililowekwa na washtakiwa huo kukidhi vigezo kutokana na kukosewa kwa hati ya mashtaka, lakini hakuwa tayari kutoa uamuzi wa kulifuta shauri hilo.

Mwenyekiti huyo wa Chadema na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo yale yanayohusika na kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya kigaidi.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa tangu miezi miwili iliyopita imekuwa ikivuta hisia za wangi ikiwamo mabalozi wa nchi za Magharibi.

Wito wa viongozi wa vyama vya siasa na jeshi la polisi watolewa

 Inspector General Polizei  Tanzania IGP Simon Sirro
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Tanzania IGP Simon SirroPicha: Police Communications Department

Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi amesema ofisi yake imepanga kuwaleta pamoja viongozi wa vyama vya siasa pamoja na jeshi la polisi kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuondoa uhasama unaojitokeza mara kwa mara.

Hata hivyo, hakubainisha bayana ni lini pande hizo zitakutana kwa ajili ya kuwa na meza ya majadiliano mbali ya kusisitiza wakuu wa vyama vya siasa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro ndiyo wataokuwa sehemu ya maridhiano hayo.

Jeshi la polisi mara kwa mara limekuwa likitupiwa lawama kwa namna linavyowabana wanasiasa kuendesha mambo yao na tukio la hivi karibuni kabisa ni lile na jeshi hilo kuuzuia mkutano wa ndani wa chama cha NCCR Mageuzi uliowahusisha wajumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho.

Muandishi: George Njogopa, DW-Dar es Salaam.