1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yakumbwa na tetemeko kubwa la ardhi

11 Machi 2011

Tetemeko kubwa la ardhi, ambalo halijawahi kutokea katika kipindi cha miaka 140 iliopita, limeyakumba maeneo ya pwani ya Kaskazini Mashariki mwa Japan leo hii (11. 03.2011).

https://p.dw.com/p/10XQr
Mionzi ya moto kutoka kiwanda cha mafuta
Mionzi ya moto kutoka kiwanda cha mafutaPicha: dapd

Taarifa za awali zinasema kuwa, tetemeko hilo la Tsunami limeshagharimu maisha ya watu zaidi ya sita, idadi ambayo inaweza kuongezeka kutokana na hali ilivyo sasa. Zaidi ya wakaazi milioni 4 wa eneo la Fukushima wanaishi pasipo na umeme.

Mashahidi wanasema tetemeko la Tsunami lenye nguvu ya 8.9 katika kipimo cha Richter, limesababisha magari, nyumba pamoja na vitu vingine kusombwa kwa pamoja katika makazi yao. Serikali ya nchi hiyo imewataka raia wahame katika maeneo ya ukanda wa pwani.

Katika mji mwingine wa Tochigi, vyombo vya habari vimetangaza kuwa jengo moja la hoteli limeporomoka, na inahofiwa idadi kubwa ya watu huenda wamefukiwa na kifusi.

Kwa ujumla, tetemeko limesababisha athari kubwa za kibinaadamu, ikiwemo watu kadhaa waliojeruhiwa.

Kituo cha basi kilichobolewa na tetemeko
Kituo cha basi kilichobolewa na tetemekoPicha: dapd

Kufutia hali hiyo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ametoa pole kwa taifa na watu wa Japan.

"Ningependa kutoa pole zetu kwa wahanga wote wa tetemeko hilo la ardhi, hususan wengi waliojeruhiwa. Bila shaka tutawasilisha pole hizi pia kwa serikali ya Japan. Wajapan ni watu wenye uzoefu wa majanga kama haya, lakini tetemeko kubwa kama hili ni pigo kubwa kwa nchi hiyo." Amesema Westerwelle.

Tetemeko hilo limelikumba pia eneo lenye vinu vya kinyuklia nchini humo, ingawa muda mfupi baadaye, Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan, alisema hakujatokea athari wala uvujaji wowote katika.

Naye msemaji wa Serikali ya Japan, Yukio Edano, alisema tayari serikali imetuma vikosi vya uokoaji katika tukio hilo, ambalo nyumba kadhaa tayari zimesombwa na maji.

Mitikisiko pia imeripotiwa katika majengo kadhaa mjini Tokyo na moto umewaka katika viwanda vya mafuta katika maeneo tofauti.

Hadi mchana wa leo (11 Machi 2011), vyombo vya habari vilikuwa vinaendelea kuripoti hali mbaya na si rahisi kutambua athari iliyotokana na tetemeko hilo, ambalo dalili zinaonesha kuwa limegharimu maisha ya watu wengi.

Waokoaji mjini Tokyo wakiwa kazini
Waokoaji mjini Tokyo wakiwa kaziniPicha: dapd

Meneja wa mkahawa mmoja wa Kichina mjini Tokyo, Hidekatsu Hata, anasema hajawahi kuona tetemeko kama hili tangu azaliwe.

Polisi nchini humo wameendela kutoa tahadhari kwa wananchi kwamba hali bado sio shwari, na kwamba tetemeko linaweza kuendelea wakati wowote.

Maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Japan, na hasa Sanriku yamekuwa yakikumbwa mara kwa mara na balaa la matetemeko ya ardhi na Tsunami ambapo tetemeko la mwisho kutokea lilikuwa la ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha Richter.

Tetemeko hilo limetishia maeneo mengine ya eneo la Asia na Pacific kama Ufilipino,Taiwan, Indonesia na Hawii, ambapo serikali husika zimekwishatoa tahadhari kwa wananchi wake.

Mwaka 1933 lilitokea tetemeko linalokaribiana na hili la 8.1 katika kipimo cha Richter, ambapo zadi ya watu elfu tatu walpoteza maisha.

Kwa ujumla, matetemeko ya ardhi ni majanga ya kawaida nchini Japan, ambayo inajumuisha zaidi ya asilimia 20 ya matukio hayo ambayo mengi yake yanakuwa ya ukubwa wa zaidi ya 6 katika kipimo cha Richter.

Mwandishi: Sudi Mnette/IPS/RTRE
Mhariri: Othman, Miraji