1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada yaanza kuwasili Chile baada ya tetemeko la ardhi

Oumilkher Hamidou2 Machi 2010

Sheria ya kutotoka ovyo,na hatua kali za usalama zimewekwa kuepusha machafuko na mali kuporowa nchini Chile

https://p.dw.com/p/MHYc
Wanajeshi wanapiga doria katika mji wa Concepcion kuwazuwia wapora maliPicha: AP

Misaada ya kimataifa imeanza kumiminika nchini Chile ambako balaa la njaa na upungufu wa mahitaji muhimu ya raia linazidisha visa vya kuporwa mali na majumba kuingia moto kufuatia tetemeko la ardhi lililogharimu maisha ya zaidi ya watu 720. Na viongozi kadhaa wa kisiasa wanawasili nchini humo kuwahani waalioathirika na zilzala hiyo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton alituwa kwa muda nchini Chile akiwa katika ziara ya Amerika ya kusini,na kuwakabidhi maafisa wa Santiago simu 20 za mkono,ikiwa ni sehemu ya mahitaji muhimu pamoja na vituo vya matibabu ya dharura na madawa ya kusafisha maji ya kunywa kwaajili ya maelfu ya wahanga.

"Wameomba wapatiwe kwa haraka vifaa vya mawasiliano,ndio maana nimeleta sehemu tuu kwanza" amesema bibi Hillary Clinton mjini Montevideo.Mjini Santiago,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amepangiwa kuzungumza na rais Michelle Bachelet na rais mteule Sebastian Pinera atakaekabidhiwa madaraka yake March 11 ijayo.

Ndege iliyosheheni misaada kutoka Brazil nayo pia inatarajiwa kuwasili hii leo,kama alivyosema rais Lula da Silva,ambae ni kiongozi wa kwanza wa kigeni kuwasili Santiago jana usiku, ili kuonyesha mshikamano pamoja na Chile.

Talca,Cauquenes na Constitucion,miji mitatu ya eneo la kati la chile iliyoathirika vibaya sana na zilzala ya jumamosi iliyopita,sheria ya kutotoka ovyo saa za usiku imetangazwa na vikosi vya usalama kuimarishwa kama ilivyotangazwa katika mji wa Concepcion tangu jumapili iliyopita,ili kuzuwia visa vya kuporwa mali na machafuko.

Machafuko makubwa zaidi yameripotiwa katika kituo kimoja cha biashara na katika duka moja kuu ambako watu wamepora mali na kuyatia moto maduka hayo jana jioni huko Concepcion-mji wa pili mkubwa na ulioteketezwa zaidi na tetemeko la ardhi la jumamosi iliyopita.Moshi unafuka bado katika eneo la kati la mji huo.

Wanajeshi elfu sabaa wamewekwa katika maeneo ya Maule na Concepcion ili kusimamia amani na kusambaza misaada-amesema rais Michelle Bachelet.

Chile Flash-Galerie Erdbeben Zerstörungen in Concepcion
Duka moja kubwa linavunjwa na wapora mali huko ConcepcionPicha: AP

"Tunajaribu kuwafikia wananchi wote wanaobidi kusaidiwa kwa njia ya baharini,angani na nchi kavu" amesema jenerali Bosco Pesse anaesimamia shughuli za kulinda utulivu na kusambaza misaada ya dharura huko Maule.

Katika baadhi ya maeneo wananchi wanaolala nje wanabeba silaha ili kulinda milki yao.

Hasara iliyosababishwa na zilzala hiyo inakadiriwa kupindukia dala bilioni 15,kiwango ambacho ni sawa na asili mia 10 ya pato la mwaka nchini humo.Hata hivyo wataalam wa kiuchumi wanaamini misingi madhubuti ya kiuchumi ya Chili itaiwezesha kujikwamua haraka .

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na Othman Miraji