1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jopo la majaji katika kesi ya Ghailani lahitilafiana

Oumilkher Hamidou16 Novemba 2010

Kizungumkuti katika kesi ya Ghailani baada ya jaji mmoja kutoa mwito aondolewe katika jopo la majaji kwa hoja msimamo wake haulingani na ule wa wenzake waliosalia

https://p.dw.com/p/QARU
Ahmed Ghailani akisikiliza kesi dhidi yake katika mahakama ya mjini New YorkPicha: AP

Jaji mmoja katika kesi ya kwanza ya kiraia dhidi ya mfungwa wa zamani wa Guantanamo, Ahmed Khalfan Ghailani. ameomba atolewe katika jopo la majaji, hatua inayoangaliwa kama mtihani mkubwa kwa upande wa mashtaka.

Katika risala aliyomtumia Jaji Lewis Kaplan, jaji huyo wa kike, anaejulikana kama jaji nambari 12, amesema uamuzi wake hauambatani na ule wa wenzake 11 wa jopo la majaji na kwamba anahisi "anahujumiwa. "Si wazi, lakini kama hoja zake zinamtia hatiani au zinataka aachiwe mtuhumiwe huyo.

Jaji Kaplan hajazungumza na jaji huyo, na amesema, hata hivyo, ni mapema mno kuingilia kati wakati majaji wanashauriana. Jopo la majaji linaendelea na mashauriano, na jaji Kaplan amekatalia mbali mwito wa wawakilishi wa mshatikiwa kutaka kesi ibatilishwe.

Kesi ya mwezi mzima ya Ghailani katika korti ya Manhattan imekuwa ikiangaliwa kama kipimo kwa mtazamo wa rais Barack Obama wa jinsi ya kuandamwa kisheria watuhumiwa 174 ambao bado wanashikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Guantanamo, nchini Cuba-ikiwa ni pamoja na Khalid Sheikh Mohammed anaetuhumiwa kuwa muasisi wa mashambulio ya kigaidi ya september 11 mwaka 2001.

Bild des ersten Guantanamo-Häftlings vor einem US - Zivilgericht Ahmed Ghailani
Ahmed Khalfan GhailanPicha: AP

Ahmed Khalfan Ghailani, mwenye umri wa miaka 36, Mtanzania anaetokea Zanzibar,anatuhumiwa kuhusika na njama ya mashambulio ya mabomu ya Al Qaida mwaka 1998 dhidi ya ofisi za ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania-mashambulio yaliyogharimu maisha ya watu 224.

"Nimeshafikia uamuzi na hauambatani na uamuzi wa majaji waliosalia", ameandika jaji huyo wa kike katika risala inayosemekana imejaa makosa ya sarufi. Amesema uamuzi wake hautobadilika, ndio maana anataka atolewe au nafasi yake apewe jaji mwengine.

Ingawa uamuzi unabidi uungwe mkono na wote, hata hivyo, jaji Kaplan amemtaka jaji huyo wa kike aendelee kushauriana na wenzake, akisema tunanukuu:"sio lazima ubadilishe uamuzi wako, kwasababu ya maoni ya majaji wengine." Mwisho wa kumnukuu jaji Lewis Kaplan.

Mwandishi: Ummil Hamidou/Reuters

Mpitiaji: Miraji Othman