1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Iraq kuukomboa mji wa Mosul

20 Februari 2015

Iraq inatakiwa ianzishe opereshini za kijeshi kuukomboa mji muhimu wa kaskazini-Mosul unaodhibitiwa na wanamgambo wa kigaidi wa dola ya kiislam IS,huku Marekani na Uturuki zikikubaliana kuwapatia mafunzo waasi wa Syria

https://p.dw.com/p/1Eeyo
PIha ya kanisa katoliki mjini Mosul iliyopigwa Novemba mwaka 2014Picha: picture-alliance/dpa

Kikosi cha wanajeshi wa Iraq na kikurdi wapatao 25 elfu wanatayarishwa ili kuweza kuukomboa mji wa Mosul unaodhibitiwa na wanamgambo wa itikadi kali wa IS. Uongozi wa kijeshi wa Marekani uliotangaza habari hizo unakadiria mji huo wa Mosul unadhibitiwa na wapiganaji kati ya 1,000 na elfu mbili wa Dola ya Kiislamu. Hakuna bado uamuzi uliopitishwa kama idadi ndogo ya washauri wa kijeshi wa Marekani watahitajika katika eneo la karibu na Mosul ili kusaidia opereshini za ndege za kijeshi dhidi ya IS.

Mosul, mji wenye wakaazi zaidi ya milioni moja ulitekwa na wanamgambo wa kigaidi wa dola ya kiislam mwezi juni mwaka jana na ni mji mkubwa kabisa kutangazwa Dola ya Kiislamu - au Khalifa, unaoanzia kaskazini ya Iraq na kupakana pia na eneo la mashariki la Syria.

Kikosi kilichotengwa kwaajili ya opereshini hizo kitaundwa na vikundi vitano vya jeshi la Iraq-uongozi wa kijeshi wa Marekani umesema.Vikosi vitatu vitatumika kama akiba na vikosi vyengine vitatu vya wapiganaji wa kikurd-Peshmerga watakuwa na jukumu la kuzuwia njia za kuingia kaskazini ya Mosul na kuwazingira wanamgambo wa IS waliopiga kambi magharibi ya mji huo.

Kikosi chengine pia kinaundwa wakihusishwa wanamgambo wa kikabila pamoja na kundi la wanajeshi watakaokuwa na jukumu la kupambana na ugaidi.

Tarehe halisi ya kuanza opereshini hizo itategemea na jinsi maandalizi yanavyoendelea upande wa Iraq.

US Kampfjets fliegen Angriffe gegen IS in Syrien Archiv August 2014
Ndege za kijeshi za Marekani zawahujumu wnamgabo wa kigaidi wa IS nchini SyriaPicha: picture-alliance/DOD/US Air Force

Ni nadra kwa jeshi la Marekani kutoa maelezo kuhusu ratiba ya opereshini za kijeshi,lakini wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imejieleza kwa kusema ripoti hii inabainisha jeshi la Iraq ni la kuaminika.

Juhudi za kuwavunja nguvu IS zimepamba moto

Marekani na Uturuki zimetiliana saini makubaliano ya kuwpatia mafunzo na vifaa vya kijeshi waasi wa Syria wanaofuata msimamo wa wastani nchini Uturuki. Habari hizo zimetangazwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglo mbele ya waandishi habari mjini Ankara. Makubaliano hayo yamekamilisha miezi kadhaa ya majadiliano magumu kati ya washirika hao wawili wa jumuia ya kujihami ya NATO kuhusu namna ya kupatiwa mafunzo waasi wa Syria na adui yupi anastahiki kulengwa.

US General James L. Terry
Jenerali wa kimarekani James L.TerryPicha: Getty Images/M. Wilson

Marekani ambayo jeshi lake la wanaanga linashiriki katika opereshini dhidi ya wanamgambo wa IS inapendelea kuwapatia mafunzo waasi ili wajiunge na mapambano dhidi ya IS. Washington inataraji mafunzo hayo yataanza kutolewa mwezi ujao wa Marchi ili kuwawezesha washirki katika mapambano dhidi ya IS hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/AP/dpa/

Mhariri: Mohammed Khelef