1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL:Raia 19 wa Korea kusini waelekea mjini Dubai baada ya kuachiwa

31 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBU1

Raia 19 wa korea kusini walioshikwa mateka na Kundi la taleban wameondoka mjini Kabul kwa ndege ya Umoja wa Mataifa na kuelekea Dubai,Emarati.Kundi hilo lilisafiri katika ndege maalum iliyokodishwa mahsusi kwa matumizi yao baada ya kuachiwa katika makundi tofauti siku ya jumatano na alhamisi.Raia hao wa Korea Kusini walizuiliwa kwa wiki sita.

Wafanyikazi hao wa misaada waliachiwa kwa awamu kuanzia siku ya Jumatano na hapo jana katika maeneo tofauti mkoani Ghazni.Ni wakati huo waliweza kufahamu kuwa wanaume wawili waliokamatwa nao Julai 19 walipigwa risasi hadi kufa.

Wanaume hao wawili kasisi mmoja wa umri wa miaka 42 na mmisheni aliye na umri wa miaka 29 walipigwa risasi katika kipindi cha majuma mawili.Kundi la Taleban lilichukua hatua hiyo ili kuishinikiza serikali kuwaachia wafungwa wao jambo lililopingwa vikali na halijatimizwa.

Kuachiwa kwa mateka hao kunatokea baada ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa kundi la Taleban na ujumbe wa Korea Kusini yaliyofanyika mjini Ghazni.Serikali ya Korea Kusini kwa upande wake imeahidi kuondoa majeshi yake 200 wanaohudumu katika vitengo vya uhandisi na utabibu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Ujerumani kwa upande wake inashtumu namna Korea Kusini ilivyosuluhisha tatozo hilo huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akishikilia kuwa nchi yake haitajadiliana na Taleban ili mhandisi wake aachiwe.Mhandisi huyo alikamatwa zaidi ya majuma 6 yaliyopita.