1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Katika Umoja huu wa Ulaya ni taabu kuendelea mbele."

Maja Dreyer13 Desemba 2007

Leo ni siku muhimu kwa Umoja wa Ulaya. Baada ya miaka mingi ya ugomvi na mazungumzo, hatimaye, viongozi wa nchi zote zanachama, leo watatia saini mkataba mpya unaofidia katiba ambayo haikukubaliwa na baadhi ya wanachama.

https://p.dw.com/p/Cb6w
Bendera za Ulaya zimepandishwa kabla ya sherehe ya leo mjini Lisbon, UrenoPicha: AP

Hata hivyo, wahariri wa magazeti hawaridhishwi na mkataba huu. Gazeti la “Tagesspiegel” la mjini Berlin lina wasiwasi ufuatauo:


“Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya wanakabiliwa na changamoto kubwa, yaani kuwaeleza wananchi wao kwa nini mkataba huu ni mafanikio licha ya kwamba si katiba. Upande mwengine hawawezi kusifu mno mkataba unaotiwa saini leo, ili raia wa Ulaya wasiamini ni kitu kipya kabisa. Yule anayetaka kuuchunguza mkataba wenyewe, atashindwa, kwani ni taabu kuuelewa kuliko ule ulioutangulia. Katika Umoja huu wa Ulaya kweli ni taabu kuendelea mbele.”


Mhariri wa gazeti la “Die Welt” pia hana furaha juu ya tukio la leo:


“Kansela wetu ameusifu mkataba huu kuwa ni mafanikio ya kihistoria. Lakini tusiikuze thamani yake. Mkataba huu mpya unaongeza demokrasia katika maamuzi ya pamoja na unapunguza uwezo wa nchi moja moja kuzuia uamuzi kupitishwa. Hii itarahisisha sera za ndani za Umoja wa Ulaya. Lakini mkataba huu hauleta hisia za umoja ndani ya Ulaya, wala suali muhimu halikujibwa, yaani mipaka ya Ulaya iko wapi?”


Gazeti la “Lübecker Nachrichten” lina maoni tofauti likiandika:

“Ulaya inaendelea kwenye njia yake ya kufanikiwa. Licha ya makosa yote yaliyofanywa na licha ya kuendelea pole pole tu, historia ya Umoja wa nchi za Ulaya tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957 ni historia ya ustawi unaokua, maendeleo bila ya mwisho na amani. Sarafu ya Euro tayari ni sarafu ya kimataifa.”


Mada nyingine muhimu duniani ni mkutano kuhusu utunzaji wa hali ya hewa unaoendelea Bali, Indonesia. Karibu kila siku, wahariri wanachunguza matokeo ya mkutano huu. Mhariri wa “Rhein-Neckar-Zeitung” leo hii ameandika hivi:


“Kuna kitu kimoja kuhusu mkutano wa Bali ambacho bado hakikueleweka. Watu wengi wanaamini, mkutano huu unalenga kuíokoa hali ya hewa kupitia uamuzi wa pamoja. Lakini si hivyo hata kidogo. Ikiwa wajumbe kutoka duniani kote wataweza kukubaliana, wataamua tu kuhusu ratiba vipi kuendelea na mazungumzo. Mafanikio yangekuwa kama nchi zinazotoa gesi nyingi chafu, ambazo ni Marekani, Ulaya, Urusi, Canada, China, India na Australia, zitakubali kupunguza.”