1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir asaini makubaliano ya amani shingo upande

Admin.WagnerD26 Agosti 2015

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ametia saini mkataba wa amani kati ya serikali yake na waasi wanaoipinga, huku akisisitiza kuwa haridhiki na yaliyomo katika mkataba huo, na kutabiri kuwa huenda hautadumu.

https://p.dw.com/p/1GLwt
Mahasimu wa Sudan Kusini; Riak Machar (kushoto) na Rais Salva Kiir (kulia).
Mahasimu wa Sudan Kusini; Riak Machar (kushoto) na Rais Salva Kiir (kulia).Picha: Getty Images/Zacharias Abubeker/Ashraf Shazly/Montage

Baada ya kuutia saini mkataba huo unaoazimia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 20 sasa nchini Sudan Kusini, chini ya shinikizo la Jumuiya ya Kimataifa, Rais Salva Kiir hakuchelewa kuukosoa mkataba huo.

Rais huyo amesema, ''Mkataba huu tunaousaini leo una vipengele vingi ambavyo hatuvikubali. Na ikiwa mashaka yetu yatapuuzwa, hali hiyo itakuwa inakwenda kinyume na maslahi ya amani ya kweli na ya kudumu''.

Kwa upande wa serikali mkataba huo umesainiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba, ukishuhudiwa na viongozi wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Upembe wa Afrika, IGAD. Viongozi hao ni pamoja na waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni miongoni mwa wengine. Walikuwepo pia wanadiplomasia wa ngazi za juu kutoka nchi na taasisi mbali mbali za kimataifa.

Machar kurejea katika wadhifa wake?

Hasimu mkubwa wa rais Salva Kiir, Riek Machar ambaye anatarajiwa kurejea katika wadhifa wa makamu wa rais kwa mujibu wa mkataba huo, aliyasaini makubaliano hayo wiki iliyopita mjini Adis Ababa.

Jumuiya ya Kimataifa imehusika pakubwa kuzipatanisha pande zinazozozana Sudan Kusini
Jumuiya ya Kimataifa imehusika pakubwa kuzipatanisha pande zinazozozana Sudan KusiniPicha: Zacharis Abubeker/AFP/Getty Images

Sudan Kusini ambayo ni nchi changa kabisa duniani ilitumbukia katika mzozo mwaka 2013, baada ya mfarakano kati ya Machar aliyekuwa makamu wa rais rais, akitoka katika kabila la Nuer, na rais Kiir ambaye anatoka katika kabila kubwa la Dinka.

Mapigano yaliyofuatia uhasama huo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, na wengine wapatao milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao.

Mikataba isiyopungua saba ambayo ilisainiwa awali baina ya pande pande hizo ilivunjika siku chache tu baada ya kutiwa saini, huku mingine ikidumu kwa masaa machache tu.

Shinikizo kutoka kila upande

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana lilionya kuwa lilikuwa tayari kuichukulia hatua serikali ya rais Salva Kiir, iwapo angeshindwa kuyaidhinisha makubaliano hayo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimeweka Sudan Kusini katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimeweka Sudan Kusini katika mgogoro mkubwa wa kibinadamuPicha: GetttyImages/AFP/C. Lomodon

Wasi wasi wa serikali ya Kiir kuhusu makubaliano ya amani aliyayasaini leo, unatuama zaidi juu ya vipengele kadhaa, kikiwemo kile kinachoitaka kuondoa shughuli za kijeshi katika mji mkuu, Juba, kuwapa madaraka makubwa waasi, na kutumiwa kwa watu kutoka mataifa ya kigeni kukagua utekelezwaji wa mkataba uliosainiwa.

Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa Ellen Marrethe Loej aliliambia Baraza la Usalama la Umoja huo jana, kwamba kuyasaini makubaliano hayo itakuwa ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye amani, akionya kuwa bado vipo vikwazo vingi njia.

Hata hivyo, Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa mkataba huo hauna budi kutekelezwa kikamilifu, na kuwataka wanasiasa mahasimu kujitahidi kupata maridhiano ya kweli, wakiweka maslahi ya wasudani kusini wote mbele ya yao binafsi kisiasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Yusuf Saumu