1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir, Machar wasaini makubaliano ya amani Khartoum

Iddi Ssessanga
27 Juni 2018

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na hasimu wake mkuu Riek Machar wamekubaliana juu ya mpango wa kudumu wa kusitisha mapigano utakaoanza katika muda wa saa 72.

https://p.dw.com/p/30PZc
Südsudan  Friedenstreffen - Präsidenten Salva Kiir und Rebellenführer Machar
Picha: Reuters/M. Nureldin Abdallah

Makubaliano  yaliosainiwa katika mji mkuu wa Sudan Khartoum yanalenga kumaliza vita ambamo mamia kwa maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni tatu kuyakimbia makaazi yao.

Makubaliano hayo ya awali yanaweka msingi wa makubaliano ya mwisho ambayo yataruhusu uwasilishaji wa misaada ya kiutu, kuachiwa huru wafungwa na kuundwa kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa baada ya miezi minne, amesema waziri wa mambo ya nje wa Sudan Al-Sirdiri Mohamed Ahmed.

Yamekuja baada ya mazungumzo yaliodumu kwa siku mbili kati ya rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar, makamu wa zamani wa rais. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilianza 2013, chini ya miaka miwili baada ya taifa hilo kujipatia uhuru wake kutoka Sudan.

"Makubaliano haya yaliosainiwa leo na usitishaji mapigano vitamaliza vita nchini Sudan kusini, na kufungua ukurasa mpya," Machar aliwaambia waandishi habari baada ya hafla ya kusaini, akifisu kile alichosema kitakuwa ujenzi wa imani na jirani wa kaskazini wa Sudan Kusini.

Äthiopien Friedensgespräche in Addis Abbea | Salva Kiir & Riek Machar
Rais Kiir (mwenye kofia) akishikana mikono na kionogzi wa waasi Riek Machar (kulia) wakati wa mazungumzo yao ya mjini Addis Ababa, Juni 21, 2018.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Ayene

Tangazo la Khartoum

Kiir na Machar wamsaini waraka, unaoitwa "Tangazo la Khartoum," mbele ya rais wa Sudan Omar al-Bashir. "Siku hii ilikuwa ikitarajiwa na watu wetu nchini Sudan Kusini na sasa imewadia," alisema Kiir baada ya kusiani makubaliano hayo. Machar aliongeza kuwa makubaliano hayo laazima yapelekee kumalizwa kwa vita.

Msukumo huu wa karibuni wa amani nchini Sudan Kusini unakuja kama sehemu ya juhudi mpya zilizoanzishwa na viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki na wakati ambapo pande hizo mbili zinakabiliwa na muda wa mwisho kuepusha vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Makubaliano kadhaa ya amani yaliofikiwa huko nyuma yalivunjika.

"Tunatoa makubaliano haya kama zawadi kwa raia wa Sudan Kusini," alisema Bashir. "Makubaliano haya yanasema amani imeanza kurejea Sudan Kusini."

Tangazo hilo, ambalo shirika la habari la Ufaransa AFP lilipata nakala yake, linasema mpango wa usitishaji mapigano unahusisha kutenga, kutenganisha vikosi vilivyo karibu, kuondoa vikosi vyote washirika, kufungua njia za kufikisha misaada ya kibindamu na kuachiwa kwa wafungwa wa kivita na wanaoshikiliwa kwa sababu za kisiasa.

Makubaliano hayo pia yanaruhusu wanachama wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya ushirikiano wa kimaendeleo baina ya serikali IGAD -- kupeleka vikosi kusimamia usitishaji wa mapigano.

"Utaratibu wa usalama ambao utatekelezwa unalenga kujenga jeshi la taifa, polisi na  vyombo vingine vya usalama shirikishi ambavyo vitakuwa huru kutokana na ukabila na uhusiano wa kikabila," unasema waraka huo. "Kutakuwepo pia na makubaliano ya kisera kuhusu kuwanyanganya silaha raia nchini kote."

Südsudan UN denken über Verstärkung von Unmiss nach
Vita vya Sudan Kusini vimesababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya raia na kuwafyana mamilioni wengine kuwa wakimbizi.Picha: Reuters/A. Ohanesian

Serikali ya mpito ndani ya miezi minne

Tangazo la Jumatano linasema serikali ya mpito itaundwa katika muda wa siku 120 ambayo itaongoza nchi kwa muda w amiezi 36. "Wakati wa kipindi hicho cha mpito nchi itajiandaa kwa uchaguzi wa kitaifa," unasema waraka huo. "Inakubaliwa kuwa uchaguzi utakuwa wazi kwa vyama vyote vya kisiasa na kuwa huru na wa haki."

Majadiliano ya mjini Khartoum yalikuja baada ya duru ya mazungumzo ilioongozw ana waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wiki iliopita kushindwa kufikia muafaka wowote.

Mazugumzo hayo ya Khartoum yalianza siku ya Jumatatu na yamepangwa kudumu kwa wiki mbili, na baadae duru inayofuata itafanyika mjini Nairobi. Duru ya mwisho inatarajiwa kufanyika Addis Ababa.

Vita vya Sudan Kusini ambavyo vimesababisha vifo vya mamia kwa maefu ya watu na kuwakosesha makaazi karibu milioni nne, vilizuka Desemba 2013 wakati Kiir alipomtuhumu makamu wake wakati huo Machar, kw akupanga njama ya mapinduzi, na kuvunja matumaini yaliofuatia uhuru kutoka Sudan miaka miwili kabla.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre

Mhariri: Saumu Yusuf