1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Afrika mwishoni mwa wiki hii

25 Januari 2008

Kamerun ina miadi leo na Chipolopolo-Zambia na lazima ishinde au irudi porini yaounde.Mabingwa Misri waonana na mamba wa mto Nile-Sudan.

https://p.dw.com/p/Cxhw

Kombe la Afrika la mataifa linaendelea leo jumamosi kwa mabingwa Misri wakiwa na miadi na jirani zao Sudan mjini Kumasi.Mafiraouni -mabingwa mara 5 wa Kombe la Afrika- waliwavunjia hadhi majuzi simba wa nyika-kameroun walipowazaba mabao 4-2.

Kocha wa Misri Hassan Shehata, anadai mabingwa Misri baada ya kuwameza simba wa nyika,hawana shida kuwatafuna mamba wa mto Nile-Sudan.

Simba wa nyika-Kameroun,watabidi leo kufuta madhambi waliofanya walipocheza na Misri. Wakikandikwa tena leo risasi na Chipolopolo-Zambia,basi itakua buriani kwa simba wa nyika na jogoo lao Samuel Eto’o litaharakisha kurudi Barcelona.

Nahodha wa Chipolopolo-Christopher Katongo ameonya kwamba chipukizi wake hawawaogopi simba wa nyika,kwani anadai simba ni chapa-chapa wamerowa maji.

Kesho jumapili, ni zamu ya timu 4 za kundi C ambamo kila moja ina matumaini ya kucheza duru ijayo:Kwanza, simba wa Terange-Senegal watawawinda paa wa Angola kabla tai wa carthage-Tunisia kuonana na Bafana Bafana-Afrika Kusini mjini Tamale:

Makucha ya simba wa nyika-kamerun wanadai baadhi ya mashabiki eti yameanza kuota kutu kama yale ya chui wa Zaire-leo simba, baada ya kutamba katika kombe la dunia.

Mabingwa hao mara 4 wa Afrika- wanaingia tena leo uwanjani kupambana na Chipolopolo-Zambia, na kukanusha hayo .Wanajua kwamba leo lazima simba wangurume na wakwepe risasi zote za Chipolopolo-risasi zilizowaua waua mamba wa mto nile walipochapwa mabao 3:0.

Zambia iliishinda Kameroun mara 3 kati ya 10 timu hizi mbili zilipokutana wakati mara 4 zilitoka sare.Kwahivyo, chipolopolo-maana risasi-zaweza kuwaumiza simba wa nyika leo jioni.

Kaburi la simba wa nyika katika kombe hili la dunia nchini Ghana lilichimbwa na Misri-mabingwa walipowakomea mabao 4:2.Ikiwa risasi za chipolopolo zitakuwa kali leo,basi zaweza kuwazika simba wa nyika katika kaburi waliochimbiwa mjini Kumasi.Zambia imetiwa moyo kwa kurudi kwenye kikosi chake kwa mastadi wake 2 waliokua wakiugua homa ya malaria.

Samuel Eto’o ndie simba pekee alienguruma pale kamerun ilipocheza na mabingwa Misri na hodi hodi zake katika lango la Misri, zilitikiwa mara 2.Leo, Eto’o anajua anabidi kupiga tena hodi hizo katika lango la zambia,kwani kama wenzao Nigeria jana walipocheza na Mali, mpambano wao leo na zambia pia ni wa kufa-kupona.

Mabingwa watetezi_misri nao wanarudi tena uwanjani leo tangu walipowazima simba wa nyika kuacha kunguruma.

Kocha wao Hassan Shehata amewataka pharoes kuionesha zaidi ufirauni wao wa dimba na wasiwastahi au kuwaheshimu majirani zao mamba wa Sudan.

Kinyume na mpambano dhidi ya Kamerun, Misri leo inacheza na nahodha wao Ahmed Hassan na mshambulizi wao hatari Mohammed Aboutrika ameshapona sawa sawa homa yake baada ya kucheza kipindi cha pili tu dhidi ya kamerun.

Nae mshambulizi wa Hamburg –klabu ya Bundesliga Mohamed Zidan ,alietia mabao 2 dhidi ya Kamerun,yutayari kutikisa wavu tena katika lango la Sudan-mabingwa wa Afrika mashariki na kati.

Mabingwa Misri wana rekodi nzuri mbele ya majirani zao wa mto nile-Sudan.KLatika mapam,bano yao 23, mafirauni wametamba mara 16 mbele ya mamba wa mto nile.Pia Misri imetia mabao 43 katika kinywa cha mamba.

Sudan itamtegemea sana mshambulizi wao mrefu Faisat Agab ambae dhidi ya Zambia hakuona wavu.Nahodha huyo wa klabu ya al Merreikh,ndie alietia mabao 5 yaliopeperusha sudan katika finali hizi za kombe la afrika baada ya kitambo cha miaka 32.

Timu ya sudan imejengeka kutoka klabu zake mbili:al Hilal na Al Merreikh na si ajabu kwahivyo, mamba hawa wanaomba dua pamoja kuwa leo iwe siku yao ya kuitikiwa dua zao.