1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kugawanyika kwa Sudan hakuepukiki

Oumilkher Hamidou6 Desemba 2010

Waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Abul Gheit amesema kugawika kwa Sudan ni swala ambalo sasa haliepukiki tena-

https://p.dw.com/p/QQVp
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Aboul Gheit (kulia)Picha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Ahmed Abul Gheit, ambaye ni mtetezi mkubwa wa Sudan moja iliyoungana , amesema jana kuwa kugawika kwa Sudan ni suala ambalo sasa haliwezi kuepukwa, ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya kura ya maoni itakayofanyika upande wa kusini mwa Sudan wakiamua kujitenga ama la.

Hali baina ya Sudan ya kaskazini na kusini inaelekeza katika kujitenga kwa upande wa kusini, amesema waziri huyo wa mambo ya kigeni katika mahojiano na televisheni ya taifa. Abul Gheit amesema kuwa , Misr imefanya mazungumzo na pande hizo mbili ili kuzishawishi kuchagua umoja badala ya mtengano, lakini kila kitu kinaashiria kuwa utengano sasa ni kitu ambacho hakiwezi kuepukwa.

Kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Januari 9 kusini mwa Sudan ni sehemu muhimu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ambayo yamemaliza miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya upande wa kaskazini na kusini ambapo watu milioni mbili wamepoteza maisha yao. Kumekuwa na juhudi chache kutoka katika pande hizo za kuendelea kuwa na umoja, amesema Abul Gheit, kuhusu Sudan, nchi ambayo ni jirani ya Misri na nchi kubwa kabisa katika bara la Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ubalozi wa Marekani mjini Cairo ambayo imetolewa mwaka jana na kufichuliwa na mtandao wa Wikileaks, Misr imeeleza hofu yake kuwa kuundwa kwa taifa la Sudan ya kusini kunaweza kuhatarisha upatikanaji wa maji ambayo ni muhimu sana kwa Misri kutoka mto Nile.

Wakati huo huo kabila moja la Waarabu ambao ni wafugaji wanaohama hama, limeteua utawala sambamba na utawala uliopo katika jimbo linalogombaniwa la Abyei, eneo ambalo linaelekea kuleta mzozo lililoko mpakani kati ya kusini na kaskazini. Mkuu wa kabila hilo la Misseriya , Mukhtar Babo Nimr ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu wa eneo hilo wameteua serikali mpya wakichukua hatua dhidi ya hatua tatu zilizochukuliwa na kiongozi wa Abyei. Amesema kuwa kiongozi wa Abyei amemteua kamishna mpya bila ya kuwashauri. Ameongeza kuwa kabila la Dinka Ngok limetangaza hawatawaruhusu watu wa kabila la Misseriya kurejea katika eneo la mto unaojukana kama Bahr al-Arab. Watu wa kabila la Missetiya ambao wameitumia ardhi ya Abyei kwa malisho ya mifugo, wametishia kuvuruga kura ya maoni iwapo hawatapewa haki sawa za kupiga kura kama kabila la Ngok Dinka, ambao ni wakulima na wanaoonekana kutaka kujiunga na upande wa kusini.

Mazungumzo baina ya kusini na kaskazini kuhusu Abyei yalivunjika nchini Ethiopia mwezi uliopita, na kusababisha maafisa wa upande wa Sudan ya kaskazini kusema itakuwa si rahisi kufanya kura hiyo ya maoni, hivi sasa ukiwa umesalia mwezi mmoja. Tume ya kusimamia kura ya maoni kwa ajili ya jimbo la Abyei haijateuliwa na pande hizo mbili zimeendelea kutofautiana kuhusiana na nani anapaswa kupiga kura katika jimbo hilo.

Mwandishi: Sekione Kitojo/ AFPE

Mhariri : Abdul-Rahman