1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Kuingilia kati C.A.R ni hatari lakini muhimu'

11 Desemba 2013

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, amesema hatua ya kupeleka wanajeshi wa Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ni hatari lakini ni muhimu ili kuzuwia umuagaji damu.

https://p.dw.com/p/1AX8r
Rais Francois Hollande akiwahutubiwa wanajeshi wa Ufaransa Jumanne jioni.
Rais Francois Hollande akiwahutubiwa wanajeshi wa Ufaransa Jumanne jioni.Picha: picture-alliance/AP

Hollande aliyasema hayo wakati alipofanya ziara fupi mjini Bangui, huku Marekani ikiahidi msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola milioni 60 kwa ajili ya nchi hiyo.

Holland aliwasili katika mji wa Bangui uliyo chini ya amri ya kutotembea usiku, baada ya kuhudhuria ibada ya kumbukumbu ya rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, na mara baada ya kuwasili, alitoa heshima za mwisho kwa wanajeshi wake waliyouawa, kwa kuinama mbele ya majeneza yao katika uwanja wa ndege wa Bangui. Hollande alisema operesheni hiyo ni hatari, lakini ni wakati wa kuchukuwa hatua, ikiwa wanataka kuepeusha mauaji.

"Katika kuingia Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ufaransa haitafuti maslahi binafsi. Haina cha kunufaika na ujio wake hapa, na haitaki kuwa na ushawishi wowote usio na sababu. Ufaransa inalenga kuleta ahueni kwa wakaazi wanaotishiwa na vikundi visivyofuata sheria," alisema Hollande wakati akiwahutubia wanajeshi wa Ufaransa walioko mjini Bangui.

Wanajeshi wa Ufaransa wakimuondoa Muislamu alietaka kuuawa na Wakrsitu wenye hasira.
Wanajeshi wa Ufaransa wakimuondoa Muislamu alietaka kuuawa na Wakrsitu wenye hasira.Picha: picture-alliance/AP

Ataka uchaguzi wa mapema
Hollande alirejea wito wake wa kutaka uchaguzi ufanyike katika nusu ya pili ya mwaka ujao, kuliko mapema mwaka wa 2015 kama ilivyokuwa imepangwa. Wakati wa ziara yake fupi, Hollande alifanya mazungumzo na rais wa muda Michel Djotodia, ambaye aliongoza uasi wa seleka ulioanza miezi 12 iliyopita. Rais huyo wa Ufaransa ambaye amemtuhumu Djotodia kwa kutofanya vya kutosha kukomesha vurugu za kidini, alikutana pia na viongozi wa dini kabla ya kuondoka.

Rais wa Marekani Barack Obama ameidhinisha kutolewa kwa dola za Marekani milioni 60 katika msaada wa kijeshi kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, fedha ambazo zitapitia kwa Ufaransa, Umoja wa Afrika na mataifa yanayochangia wanajeshi kwa vikosi vya kimataifa chini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ingawa jeshi la Ufaransa linasema kwamba wanamgambo wengi wamekwisha nyanganywa silaha, changamoto halisi ni kuzuwia hasira za Wakristu dhidi ya Waislamu. Shirika la Amnesty International limeripoti kuongezeka kwa mashambulizi ya kidini ambapo misikiti na nyumba za Waislamu vimechomwa moto.

Rais wa muda wa C.A.R Michel Djotodia.
Rais wa muda wa C.A.R Michel Djotodia.Picha: Getty Images

Vurugu za kijamii
"Tatizo kubwa sasa ni kwamba kila siku iendayo kunakuwa na matukio mapya na hali za kutisha. Wiki iliyopita,yalikuwa ni mapigano kati ya watu wenye silaha, sasa ni mapigano kati ya jamii, alisema Christin Musoka, mfanyakazi wa Amnesty Inernational nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Shirika la misaada la Msalaba mwekundu, jana Jumanne limekusanya maiti zaidi y a100 na kuzipakia kwenye malori kwa ajili ya maziko katika kaburi la pamoja katika eneo la Bimbo mjini Bangui. Kamishna na wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, aliripoti jana kuwa karibu watu 108,000 wameyakimbia makaazi yao mjini Bangui pekee, wakiamua kulala nje kuliko kuhatarishia maisha yao majumbani.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,dpae, rtre
Mhariri: Hamidou Oummilkheir