1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni yaendelea kusini mwa Sudan

Sekione Kitojo11 Januari 2011

Kura ya maoni imeendelea kufanyika katika eneo la kusini mwa Sudan licha ya mapigano ya kikabila yaliyosababisha watu 23 kuuwawa katika jimbo la Abyei.

https://p.dw.com/p/zw53
Wapiga kura wa kusini mwa Sudan wakiwa wamesimama katika mstari tayari kwa kupiga kura.Picha: picture alliance/dpa

Kura ya  maoni  nchini  Sudan  kuhusu   eneo  la  kusini lijitenge  ama  la  imeendelea  kuwa  na  milolongo  mirefu ya  wapiga  kura  katika  siku  yake  ya  pili  lakini imechafuliwa  pia  na  mivutano  ambayo  imesababisha maafa   katika  jimbo  la  Abyei. Machafuko  hayo yamesababisha  kiasi  watu  23  kupoteza  maisha  tangu siku  ya  Ijumaa. Vikosi  vya  kulinda  amani  vya  umoja  wa mataifa  vimepelekwa  katika  eneo  hilo  kufanya uchunguzi  katika  jimbo  la  mpakani, ambako  kura  ya maoni  kuhusu  hatma  ya  eneo  hilo  imeahirishwa. Viongozi  wa   kabila  la  Dinka, ambao  wanapendelea kuwa  upande  wa  kusini, wameishutumu  serikali  ya upande  wa  kaskazini  mjini  Khartoum  kwa  kuwapa silaha  Waarabu  wafugaji  katika  jimbo  la  Abyei. Msemaji wa   jeshi  la  Sudan  ya  kaskazini   amekanusha kuhusika  kwa  aina  yoyote  na  machafuko  hayo. Kwingineko  nchini  Sudan , jana  Jumatatu, maelfu  ya wapiga  kura  walijipanga  kwa  amani   kupiga  kura. Kura hiyo  ya  maoni  itafanyika  kwa  muda  wa  wiki  nzima. Ni kilele  cha  makubaliano  ya  amani  ya  mwaka  2005 ambayo  yamemaliza  miongo  miwili  ya  vita  vya wenyewe  kwa  wenyewe  katika  nchi  hiyo  yenye  utajiri mkubwa  wa  mafuta.