1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya Sudan mtihani kwa Obama

Mwandishi:Martin,Prema/RTRE5 Januari 2011

Kura ya maoni itakayopigwa Sudan ya Kusini siku ya Jumapili, ni mtihani mpya kwa sera za kidiplomasia za Marekani katika kanda hiyo.

https://p.dw.com/p/Qnfv
Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: dpa

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, litakuwa pigo kubwa sana kwa Rais Barack Obama, ikiwa machafuko mapya yatazuka baada ya kura hiyo ya maoni. Marekani, kwa tahadhari, inaamini kuwa kura hiyo ya maoni, itakwenda kwa usalama, ikitabariwa kuwa Wasudan wa Kusini wataamua kujitenga na serikali ya Kaskazini na hivyo kuunda taifa lao huru. Kura hiyo ya maoni, ni sehemu muhimu ya mkataba wa amani wa mwaka 2005, uliomaliza umwagaji mkubwa kabisa wa damu barani Afrika.

Kwa maoni ya mwanaharakati wa haki za binadamu,John Prendergast, miezi sita ya mwanzo kufuatia kura hiyo ya maoni, ni kipindi cha hatari. Anasema, Obama huenda akakumbana na yale yaliyomkabili rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton. Clinton amewahi kutamka kuwa juto lake kuu kama rais, ni kushindwa kuzuia mauaji ya watu 800,000 katika mgogoro wa Sudan.Katika jitahada za kuzuia hatima kama hiyo,Washington miezi ya hivi karibuni ilikuwa mbioni kuzuia mivutano kati ya serikali kuu mjini Khartoum na viongozi wa Sudan ya Kusini mjini Juba.

Lakini Marekani inawasiwasi na kipindi cha mpito cha miezi sita kufuatia kura hiyo ya maoni. Je, isaidie kwa njia gani ili kuhakikisha amani kati ya Kaskazini na Kusini, pande zinazotofautiana kwa dini, kabila,itikadi na hata kuhusu mapato ya mafuta.Kwa maoni ya Prendergast, Marekani itakuwa na dhima muhimu kufuatia kura hiyo ya maoni.Kwani katikati ya mwaka jana, Washington ilijitosa kushughulikia suala la Sudan kwa kutoa vivutio. Kwa mfano, hatimae kurejesha uhusiano wa kawaida na Sudan ikiwa itaruhusu kura hiyo ya maoni kupigwa. Vile vile ikampeleka mwanadiplomasia wa zamani Princeton Lyman kuongoza binafsi mazungumzo kati ya Kaskazini na Kusini. Marekani imekosolewa kuregeza msimamo wake, lakini serikali ya Obama imeamini kuwa haitosaidia kuchukua hatua kali tangu mwanzoni.

Na baada ya Rais Omar al-Bashir hiyo jana, kuahidi kuwa ataheshimu matokeo ya kura ya maoni itakayopigwa Jumapili ijayo, maafisa wa Marekani wanasema, jitahada zao za kidiplomasia zimezaa matunda - angalao kwa hivi sasa. Hata hivyo, Marekani inakabiliwa na changamoto kali kumaliza tofauti zilizobaki kati ya Kaskazini na Kusini, hasa kuhusu jimbo la mpakani la Abyei lenye utajiri wa mafuta.

Wengi wana wasiwasi kuwa eneo hilo ni tishio kubwa kwa amani ya kudumu. Marekani haina budi kuhakikisha kuwa jumuiya ya kimataifa itakuwa na msimamo mmoja na hasa miongoni mwa majirani wa Sudan, ili makubaliano ya hivi sasa yapate kutekelezwa kwa amani, huku ikitafutwa njia ya kuligawa taifa kubwa kabisa barani Afrika. Kwani ni wengi wanaoamini kuwa wakaazi wa Sudan ya Kusini wataamua kujitenga na hivyo litazaliwa taifa jipya.