1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lieberman asema hakuna matumaini ya kuundwa taifa la Palestina kufikia 2012

Josephat Nyiro Charo29 Juni 2010

Wakati huo huo, Israel imekosolewa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu kwa mpango wake kutaka kuyavunja makaazi ya Wapalestina huko Jerusalem Mashariki

https://p.dw.com/p/O68Z
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Israel, Avigdor LiebermanPicha: AP

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Avigdor Lieberman, amekutana leo na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavron, mjini Jerusalem. Lieberman amesema haoni uwezekano wa nchi yake kutimiza ndoto ya jumuiya ya kimataifa ya kuundwa taifa la Wapalestina katika kipindi cha miezi 18 ijayo.

Waziri Lieberman amesema ukweli halisi kuhusu mchakato mzima wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati ni kwamba bado wangali mbali mno kufikia makubaliano ya kuundwa taifa huru la Palestina kufikia mwaka 2012. Kiongozi huyo wa Israel ameyasema hayo akiwa ameandamana na mwenzake, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye analizuru eneo la Mashariki ya Kati.

Pande nne zinazoshughulikia juhudi za amani ya Mashariki ya Kati, zikiwemo Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Urusi, mnamo mwezi Machi mwaka huu zilitaka kufikiwe mkataba wa amani katika kipindi cha miezi 24 utakaowezesha suluhisho la mataifa mawili.

Lieberman amezungumza na waziri Lavrov kuhusu mazungumzo ambayo si ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina yanayosimamiwa na Marekani, yaliyoanzishwa mwezi Mei mwaka huu, kufuatia miezi kadhaa ya jitihada za kidiplomasia zilizofanywa na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, George Mitchell, ambaye amerejea katika eneo hilo hii leo.

Russland Aussenminister Sergej Lawrow
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei LavrovPicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kukosekana ufanisi kwenye mazungumzo ya kutafuta amani kunachochea itikadi kali miongoni mwa Wapalestina na kuongeza kwamba ana matumaini mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina yatasaidia kuanzishwB mazungumzo ya ana kwa ana hivi karibuni.

Miongoni mwa wanachama wa pande nne zinazohusika na mchakato wa kutafuta amani Mashariki ya Kati, ni Urusi pekee ambayo kwa uwazi ina mawasiliano na chama cha Hamas kinachoutawala Ukanda wa Gaza, chama ambacho kimeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, ameutembelea pia Ukingo wa Magharibi, ambako amekutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, mjini Ramallah. Akiwa huko Bwana Lavrov amesema Wapalestina watapokea magari 50 ya kivita kutoka Urusi ambayo yalikuwa yamekwama nchini Jordan, na yatawasili katika siku chache zijazo. Viongozi wa wizara ya ulinzi ya Israel pamoja na jeshi la nchi hiyo hawajasema lolote kuhusu magari hayo. Mnamo mwaka 2008 Israel iliidhinisha usafirishaji wa magari hayo na wizara ya ulinzi ya Urusi, lakini kuwasili kwao kumekuwa kukicheleswha mara kwa mara.

Wakati haya yakijiri, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za binadamu, Richard Falk, ameikosa Israel kwa mpango wake wa kutaka kuyavunja makaazi ya Wapalsetina katika eneo la Silwan huko Jerusalem Mashariki. Amesema mpango huo si halali na unadhihirisha juhudi za kimkakati za Israel kuwafukuza Wapalsetina kutoka mji huo mtakatifu. Bwana Falk amesema mpango mwingine wa Israel kutaka pia kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki hadi eneo la Ukingo wa Magharibi huenda ukawa kosa la uhalifu wa kivita.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Miraji Othman