1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lissu: Natamani kuwaona tena Watanzania

Sudi Mnette
7 Septemba 2018

Siku kama ya leo (07.09.2017) majira ya saa 7 mchana katika makao makuu ya Tanzania, Dodoma kulifanyika shambulio la fedhea, ambapo mbunge wa Mbunge wa Singida ,Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi.

https://p.dw.com/p/34TPE
Tundu Lissu - Politiker aus Tanzania im Krankenhaus von Nairobi
Picha: Chadema

Ulikuwa mkasa wa  kufyatuliwa risasi 38 nje ya nyumbani kwake eneo lijukanalo kama Area D mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka katika kikao cha Bunge na baadae kukimbizwa kwa ajili ya kunusuru uhai wake katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kisha kuhamishiwa jijini Nairobi, Kenya alikotibiwa kwa takribani miezi miwili, kupelekwa nchini Ubelgiji.

Mwaka mmoja baadae akiwa nyumbani kwake mjini  Tienen nje kidogo ya jiji la Brussels,  Lissu alifanya mazungumzo na DW kwa takribani dakika 30. Katika mazungumzo hayo amezungumza mengi kuhusu afya yake, huku akionesha kuwa mwenye matumaini mengi akisema atapona na kurejea katika shughulizi zake za kisiasa.

Tundu Lissu - Politiker aus Tanzania im Krankenhaus von Nairobi
Mwanasiasa Tundu Lissu alipokuwa NairobiPicha: Chadema

Nani kamshambulia Lissu

Hadi sasa imekuwa kitendawili kwa vyombo vya usalama  nchini Tanzania. Kuhusu suala hilo Lissu alisema "Hilo ni swali gumu kidogo, kwa sababu niliposhambuliwa, lilikuwa jambo la haraka sana, sidhani kama ilichukua dakika tatu, wakakimbia nikakimbizwa hospitali.” Utata wa hali yake kwa wakati huo ndio uliosababisha   ahamishwe hospitali nyingne mjini Nairobi Kenya. Na kwa takribani juma zima hakuwa na fahamu, aliweza kuanza kutambua na kujielewa akiwa hospitalini Nairobi, Kenya.

Itakumbukwa wakati mkasa huo, ukimfika Lissu alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), na kiongozi mwenye kusimamia masuala ya kisheria katika chama chake CHADEMA. Lissu kwa nafasi yake alikuwa mtetezi wa matatizo ya kisheria kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini Tanzania. Mbali ya masuala ya kisiasa hata ya kijamii kwa makundi ya watu katika mazingira yanayowazunguka.

Risasi 16 ziliingia mwilini

Katika shambulizi hilo, Lissu alifyatuliwa risasi 38, zilizongia mwilini 16 na hadi sasa kafanyiwa upasuaji mara 21. Gari iliyohusishwa na mkasa huo ilifuata nyuma, wakati akielekea nyumbani kula chakula cha mchana baada ya mkutano wa bunge. Eneo ambalo, mwenyewe Lissu anasema kwa kawaida lina ulinzi mkali. Dereva wake alifanikiwa kuruka na kujificha chini ya gari, huku yeye akisalia katika mazingira ya kumiminiwa kiwango kikubwa cha risasi.

Alipigwa risasi tatu mbili kwenye paja la kushoto na kupitiliza kutokea upande wa pili, Alipigwa risasi tatu juu kidogo ya kiuno, upande wa kushoto zilikwaruza ngozi ambazo hazikumsababishia madhara makubwa, risasi mbili mkono wa kushoto chini ya kiwiko na kwenye kiwiko chenyewe na risasi moja kwenye mkono wa kulia chini ya kiwiko. Mikono yote miwili ilivunjika. Kwa upande wa kulia, alipigwa risasi moja kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia ambayo iliuvunja mfupa huo vipande vipande. Risasi nyingine ilivunja mfupa wa nyonga.

Risasi iliyosalia kwenye uti wa mgongo

Baadae hospitalini Dodoma na Nairobi, madaktari walifanikiwa kutoa risasi sita tumboni na moja kwenye kiwiko cha mkono wa kushoto. Risasi moja imebaki chini ya uti wa mgongo juu kidogo ya kiuno. Risasi hiyo imekaa sehemu nyeti na haiwezi kutolewa kwa sasa kwa hivyo kwa mujibu wa kitabibu, hatiakuwa na madhara na anaweza kushi nayo kwa wakati wake wote. Majeraha yaliyotokana na risasi hizo yalikuwa makubwa sana.

Katika mazungumzo yake Lissu alihitimisha kwa kusema mwaka huu umekuwa mrefu sana sio kwa sababu ya majeraha aliyonayo mwili. Ni kwamba anaikumbuka sana Tanzania pamoja na Watanzania. Anakumbuka harakati zake bungeni, licha ya kile alichokisema matatizo yote yanayotajwa sasa. Aidha anawakumbuka na kutamaani kuwaona wapiga kura wake wa Jimbo la Singida Mashariki na mikutano yetu ya hadhara, "Nime-miss sana mapambano ya utetezi wa haki za watu wetu ndani na nje ya Mahakama. Nimewa-miss mawakili wa Tanzania Bara walionipa heshima ya kuwaongoza katika kipindi kigumu sana katika historia ya TLS. Mshairi Sipho Sepamla aliandika shairi lingine liitwalo 'The Exile', yaani 'Uhamishoni.' Shairi hilo linaelezea machungu ya kuishi uhamishoni kwa kulazimishwa wakati wa utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini." Hata hivyo Lissu anasema atarejea nyumbani Tanzania baada afya yake kuwa vyema.

Mwandishi: Sudi Mnette

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman