1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kuweka chini silaha Syria yaandaliwa

Oumilkheir Hamidou
29 Desemba 2016

Urusi na Uturuki zinataka kuhakikisha makubaliano ya kuweka chini silaha yanatekelezwa Syria kabla ya mwanzo wa mwaka mpya. Habari hizo zimetangazwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlüt Cavusoglu.

https://p.dw.com/p/2Uznn
Syrien Ras al Ayn - Ausstellung Conflict
Picha: A. Spyra

Katika mahojiano na kituo cha matangazo cha Ahaber, Cavusoglu ameongeza kusema kwamba makundi yote ya wanamgambo wa kigeni wanaopigana nchini Syria-ikiwa ni pamoja na Hisbollah, watabidi waihame nchi hiyo. Taarifa yake imesadifu siku moja baada ya Uturuki kusema viongozi wa nchi hiyo na wale wa Urusi wanaandaa makubaliano ya kuweka chini silaha.

"Tunakarubia kufikia makubaliano pamoja na Urusi. Ikiwa kila kitu kitapita vizuri, makubaliano yatapatikana. Urusi itakuwa mdhamini wa serikali" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu na kuongeza makubaliano yataanza kufanya kazi kabla ya mwaka mpya.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki amesisitiza hata hivyo mazungumzo ya Astana kati ya Uturuki na Urusi hayakinzani na yale yaliyokuwa yakisimamiwa na Umoja wa Mataifa mjini Geneva. "Ni hatua ziada", amesisitiza.

Wanajeshi wa Syria wanapumzika baada ya kuukomboa mji wa Aleppo
Wanajeshi wa Syria wanapumzika baada ya kuukomboa mji wa AleppoPicha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Kitisho cha mazungumzo kuingia ukorofi

Urusi na Uturuki ni wadhamini wa makubaliano hayo yaliyofikiwa mjini Ankara. Bado haijulikani kama Iran itatia saini makubaliano hayo kama mdhamini. Wapiganaji wote watabidi waihame Syria. Hisbollah watabidi warejee Libnan", amesisitiza.

Matamshi ya Cavusooglu yanaonyesha ishara ya maendeleo katika mazungumzo yaliyolengwa kufikia makubaliano ya kuweka chini silaha. Hata hivyo shinikizo la viongozi wa mjini Ankara kutaka Rais wa Syria Bashar al Assad ang'atuke, linaweza kukorofisha mazungumzo pamoja na mshirika mkubwa wa rais huyo-Urusi.

Na madai kwamba wanamgambo wa kishia wa Hisbollah waihame Syria na kurejea Libnan, hayatowafurahisha pia wa Iran-washirika wengine wakubwa wa Rais Assad.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu (kushoto) na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrow
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu (kushoto) na mwenzake wa Urusi Sergei LavrowPicha: picture-alliance/dpa/M. Shipenkov

Urusi na Uturuki zinajongeleana

Makundi muhimu ya waasi yalikuwa yakijadiliana na Uturuki kuhusu pendekezo la kuweka chini silaha lililofikiwa kati ya Uturuki na Urusi. Makundi hayo lakini yalilikataa pendekezo la Moscow la kutoihusisha ngome ya waasi karibu na mji mkuu na aina yoyote ya makubaliano.

Kabla ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki kutoa habari hizo, Labib Nahhas, ambae ni mkuu wa tume ya uhusiano na nchi za nje wa kundi la waasi wa Syria-Ahrar al-Cham amethibitisha kupitia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya Urusi na Uturuki kuhusu mpango jumla wa kuwekwa chini silaha nchini Syria.

Ingawa Urusi na Uturuki zina misimamo inayokinzana kuelekea vita vya Syria, hata hivyo nchi hizo mbili zimeanza kujiongelea miezi michache iliyopita na kushirikiana kwa lengo la kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Syria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo