1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa ya toa wito wa utulivu Mali

Saleh Mwanamilongo
13 Julai 2020

Shughuli za kibiashara zimesimama Jumatatu mjini Bamako, ambako benki pia hazikufunguliwa.Lakini usafiri ulirejea baada ya waandamanaji kulazimika kuondoka kwenye maeneo kadhaa ambako walikuwa wakiandamana kwa vurugu.

https://p.dw.com/p/3fGRG
Maandamano ya vurugu  mjini Bamako,Mali ilikuomba rais Keita ajiuzulu.
Maandamano ya vurugu mjini Bamako,Mali ilikuomba rais Keita ajiuzulu.Picha: Getty Images/AFP/M. Cattani

Jumuiya ya kimataifa imetowa wito wa kuachiwa huru viongozi wa maandamano nchini Mali katika juhudi za kupunguza ghasia. Mwishoni mwa wiki iliyopita maandamano ya vurugu ya kumtaka Rais Ibrahim Keita kujiuzulu, yalishuhudiwa katika mji mkuu, Bamako na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 11.

Shughuli za kibiashara zimesimama leo Jumatatu mjini Bamako, ambako benki pia hazikufunguliwa. Lakini usafiri ulirejea baada ya waandamanaji kulazimika kuondoka kwenye maeneo kadhaa ambako walikuwa wakiandamana kwa vurugu.

Hayo ndiyo machafuko mabaya zaidi kuwahi kulikumba taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya miaka mingi. Hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa katika mitaa ya mji huo hapo jana, wakati mamia ya watu walikusanyika kuhudhuria mazishi ya waandamanaji wanne waliouawa. Modibo Kadioke, mmoja ya viongozi wa waandamanaji anasema Rais Keita bado hajayapatia ufumbuzi madai yao.

''Mageuzi yanayohitajika nchini Mali ni makubwa na ni mengi ambayo hatuwezi kuyapatia ufumbuzi. Kamwe hatuwezi kufanya mageuzi hayo katika nchi iliogawanyika''.

Kwenye taarifa ya pamoja wajumbe wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Uchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya nchini Mali waliomba kuachiwa huru kwa viongozi wa maandamano. Wajumbe hao walielezea wasiwasi wao na kuziomba pande zote kujizuia na machafuko. Walilaumu vikali umwagikaji damu, hasa upande wa serikali ambayo vikosi vya usalama vilitumia silaha dhidi ya waandamanaji. Walioshuhudia walisema maafisa wa polisi walifyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji

Waandamanaji waendelea kumtaka rais ajiuzulu

Imam Mahmoud Dicko ,Kiongozi wa waandamanaji nchini Mali.
Imam Mahmoud Dicko ,Kiongozi wa waandamanaji nchini Mali.Picha: Reuters/M. Rosier

Zaidi ya wapinzani 20 walikamatwa toka Ijumaa wakiwemo viongozi wa maandamano ya kutaka kujiuzulu kwa Rais Keita. Kiongozi wa maandamano nchini Mali, ambaye pia ni kiongozi wa kidini, Imam mwenye ushawishi mkubwa Mahmoud Dicko, alitoa wito wa kuwepo utulivu jana Jumapili. Hali ya wasiwasi iliendelea kushuhudiwa katika mitaa ya mji huo hapo jana, wakati mamia ya watu walipokusanyika kuhudhuria mazishi ya waandamanaji waliouawa.

Maandamano hayo katika miji kadhaa ya nchi, yalisababisha kuundwa kwa vuguvugu la M5, linalowajumuisha viongozi wa kidini, wa kisiasa na wale wa asasi za kiraia, liloanzisha maandamano tangu mwanzoni mwa mwezi Juni.

Katika juhudi za kumaliza maandamano nchini mwake, Rais Keita alitangaza kuunda serikali ya mseto na kuivunja mahakama ya kikatiba, ambayo uamuzi wake wa kubatilisha matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu, ulikuwa kiini cha maandamano hayo. Licha ya tangazo hilo la Rais Keita, viongozi wa waandamanaji wanaendelea kumtaka ajiuzulu.

Rais Ibrahim Boubacar Keita mwenye umri wa miaka 75, ameiongoza Mali tangu mwaka 2013, baada kushinda katika uchaguzi wa kuiongoza nchi hiyo kwa muhula w pili mwaka 2018.