1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kimya kingi kisicho mshindo China

4 Juni 2014

Kumbukumbu ya vuguvugu la kidemokrasia la 1989 zinavunjwa kwa mfumo maalum na Chama cha Kikomunisti kinachohofia kwamba China iliyo huru zaidi bado inawezekana kama anavyosema Matthias von Hein.

https://p.dw.com/p/1CBu1
Matthias von Hein wa Idhaa ya Kichina, Deutsche Welle.
Matthias von Hein wa Idhaa ya Kichina, Deutsche Welle.Picha: DW

"Mwenye kuidhibiti jana, anaidhibiti kesho. Anayeidhibiti leo, anaidhibiti kesho." Ni sentensi kwenye riwaya iitwayo "1984" ya George Orwell, inayoakisi kuporomoka kwa dola ya kiimla.

Sentensi hii pia inaakisi sana namna uongozi wa China unavyoendelea kuuelezea ukandamizaji miubwa dhidi ya vuguvugu la kidemokrasia uliofanyika robo karne iliyopita.

Serikali ya China inaweka wazi kwamba inahimiza udhibiti wake kwa mambo ya leo. Hairuhusu aina yoyote ya historia ambayo inatafautiana na ile ya iitwayo rasmi.

Kwa mujibu wa serikali, kilichofanyika usiku wa tarehe 3 hadi 4 Juni 1989 kilikuwa ni kuzima vuguvugu la kupinga mapinduzi kwa ajili ya kurejesha utulivu na kuzima machafuko.

Ni marufuku kukumbuka kwamba miaka 25 iliyopita, mamilioni ya watu waliandamana mjini Beijing na miji mingine kudai uhuru wa kujieleza, dhamira na utawala wa sheria, ama kwa ufupi, demokrasia.

Kimya, kimya, kimya tu

Kuna ukimya juu ya ukweli kwamba siku hizo 52 za maandamano katika majira ya machipuko ya mwaka 1989, zilikuwa za amani na zisizo fujo. Kuna ukimya pia juu ya mapambano ya kugombea madaraka ambayo yalikuwa yakiendelea wakati huo kwenye tabaka tawala.

Kimya juu ya ukweli kwamba baada ya wenye msimamo mikali kushinda vita hivyo vya madaraka, jeshi lilitumwa kuwauwa watu wao wenyewe.

Kila kitu kuhusiana wimbi hilo la mageuzi la mwaka 1989 ni miko kulisema. Umma mzima wa China umelazimishwa kuwa na maradhi ya kusahau. Kikosi kizima cha kisiasa kimetumwa kupambana na yeyote anayepambana na jaribio hili la kuidhibiti jana.

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limekusanya orodha ya wale ambao wamewekwa kizuizini au kwenye kifungo cha nyumbani kwa kuhusishwa na kumbukumbu hizi za leo.

Ya 1989 yamesahauliwa

Hivi leo, ni shida kumkuta mtu anayeweza kukisia mageuzi ya kisiasa ambayo tawi la wenye msimamo wa wastani kwenye Chama cha Kikomunisti walitaka kuyaanzisha kabla ya kuangushwa kwake mwaka 1989.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Zaho Ziyang, alikuwa ameweka uhuru wa vyombo vya habari kwenye ajenda, na hata kukitenganisha chama na serikali. Yote hayo yalipondwapondwa na vifaru kwenye Uwanja wa Tiananmen.

Kikiwa chini ya uongozi wa Deng Xiaoping wakati huo, Chama cha Kikomunisti kiliamua kuwa dhidi ya uhuru na kuwa kwa maslahi ya udikteta na ukandamizaji.

Lengo muhimu kabisa na la pekee lilikuwa ni kuhakikisha kuwa chama hicho kinaendelea kutawala. Kwa hilo, kikatelekezea misingi yake yote ya kiitikadi na kuwa chama cha ubepari wa dola.

Ombwe hili la kiitikadi lilikuja kujazwa na utaifa – na fursa ya kujitajirisha. Mtazamo huu wa kisiasa ulichochea miujiuza ya kiuchumi, bali pia ukachochea ufisadi ambao ulikwenda hadi kwenye viongozi wa juu wa chama. Ukatengeneza jamii yenye pengo kubwa kabisa la utajiri duniani.

Na matokeo yake umewacha mazingira yaliyoharibiwa na kuchafuliwa.

Mwandishi: Matthias von Hein/Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman