1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Vyeo vya Rais Samia visiwachanganye Watanzania

Grace Kabogo
28 Machi 2021

Hivi karibuni Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania. Mjadala umeibuka iwapo aitwe ''Mama Samia'' au la. Mama ni kuonesha heshima, haipunguzi mamlaka yake ya urais anaandika Grace Kabogo.

https://p.dw.com/p/3rHsB
Tansania | Amtseinführung Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP Photo/picture alliance

Baadhi ya Watanzania wameamua kumuita Rais Samia Suluhu Hassan 'Mama Samia'. Wengine wanasema watu hawapaswi kutumia neno hilo kwa kiongozi wa nchi kwani hata marais wanaume waliopita hawakuitwa baba. Kwa vyovyote vile, hakuna mtu anayepaswa kuonekana hana heshima kwa kumuita rais mpya wa Tanzania Mama Samia

Kwangu mimi, mama ni kiongozi, mlezi, mtu anayejali, mnyenyekevu, mpole na mwenye upendo kwa watoto wake. Ingawa baadhi ya wanaharakati wanawake wanaamini kuwa linapokuja suala la uongozi tena kwa kuzingatia katiba, sheria na kanuni zilizopo katika nchi neno mama halipaswi kuwepo.

Wako wanaodai kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakililia usawa kutaka kuondoa mfumo dume katika jamii. Hivyo mama linapotumika tunabaki palepale kwenye kujitambulisha kwa kutumia jinsia ya ''kike'', ingawa kwangu si hoja.

Mama Samia tangu akiwa makamu wa rais

Neno Mama Samia sio geni. Tangu akiwa makamu wa rais chini ya utawala wa Hayati John Pombe Magufuli 2015, watu walikuwa wakimuita Mama Samia. Sikuwahi kusikia akilalamika kuitwa hivyo. Hata hivyo, wako wanaosema anatakiwa kuitwa mama akiwa nyumbani na kazini anapaswa kuitwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kommentarbild Grace Kabogo
Grace Kabogo wa Idhaa ya Kiswahili ya DW Picha: Laila Richardson/DW

Bila shaka ni jambo geni kwa Tanzania, kwa sababu ndiyo mara ya kwanza taifa hilo la Afrika Mashariki kupata rais mwanamke. Maendeleo haya ya kisiasa yanaripotiwa kuwafanya baadhi ya wakosoaji kuhoji kuhusu uwezo wake wa uongozi. Rais Samia mara moja aliwatoa hofu wale wasioamini kama ataweza.

Akihutubia katika shughuli ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Magufuli Machi 22 mjini Dodoma, Rais Samia alielezea utayari wake na nia ya kuliongoza taifa la Tanzania na kuwataka watu wasiwe na wasiwasi kwani hakuna kitakachoharibika chini ya uongozi wake. ''Kwa wale ambao wana mashaka mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Tanzania, nataka niwaambie kuwa aliyesimama hapa ni rais. Narudia, nimesimama hapa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye maumbile yake ni mwanamke,'' alisisitiza rais huyo.

Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere hadi leo anaitwa Mwalimu Nyerere. Je hii ilikuwa ni kumkosea heshima? La hasha! Na zaidi ya hapo - kiongozi wa kwanza mwanamke wa Afrika aliyechaguliwa kidemokrasia - rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf aliitwa ''Mama wa Liberia.''

Jinsi ya kumtambulisha Amiri Jeshi Mkuu.

Mbali na neno Mama, utata mwingine ulioibuka wa jinsi ya kumtambulisha Rais Samia ni ''Amiri Jeshi Mkuu''. Sababu sasa tuna rais mwanamke, hoja iliyopo ni kutokana na baadhi kusema Rais Samia atambulishwe kama Amira Jeshi Mkuu au Amirat Jeshi Mkuu, na sio Amiri Jeshi Mkuu.

Neno Amiri limetoholewa kutoka kwenye lugha ya Kiarabu lenye maana ya ''kiongozi mkuu mwanaume.'' Neno hili linaonesha mamlaka ya kwamba rais ndiyo anatoa amri kwa majeshi yote nchini ya ulinzi na usalama. Kwa sababu lugha ya Kiswahili haina jinsia ya Kiume au Kike hili limezusha mjadala mkubwa.

Lakini Ijumaa ya Machi 26, wakati Hayati Magufuli anazikwa huko Chato, Geita, Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo aliumaliza utata huo kwa kusema Rais Samia anatambulishwa kama Amiri Jeshi Mkuu.

Wachambuzi na wakaazi waelezea matarajio yao katika utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan

Sidhani kama kumuita Rais Samia Amiri Jeshi Mkuu tutakuwa tunauhusisha urais wake na jinsia ya kiume. Tusiyafanye mambo kuwa magumu zaidi, badala yake tubaki na Kiswahili chetu ambacho hakina jinsia.

Matumizi ya jina la mwisho

Kama hilo halitoshi, kuna mengi yanayozungumzwa tangu Rais Samia alipoapishwa kuiongoza Tanzania. Matumizi ya jina la mwisho kwa viongozi nao ni mjadala mwingine. Tumeshuhudia marais waliopita wa Tanzania wakiitwa kwa majina yao ya mwisho, kwa mfano Rais Mwinyi, Rais Kikwete na kadhalika.

Lakini sasa tuna rais mwanamke, je tumuite Rais Samia au Rais Hassan? Kwa kuitwa hivyo, bila shaka masikioni mwa watu jina hilo litasikika la jinsia ya kiume.

Tansania Daressalam | Amtseinführung neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan pia ni Amiri Jeshi MkuuPicha: STR/AFP/Getty Images

Au tumuite Mheshimiwa Rais au Mama Samia au Mheshimiwa Rais Mama Samia? Huo ni uhuru wa kila mmoja anavyojisikia, ili mradi tu mipaka isivukwe na heshima yake ibaki pale pale kama rais wa nchi.

Tukirejea kwa Mama ni jina la heshima kubwa, lakini halina maana kama Tanzania haitokuwa imeungana, haitokuwa na demokrasia, uhuru wa kujieleza, utawala bora au iwapo sheria kandamizi hazitarekebishwa. Jina mama litakuwa na heshima endapo ataongoza kwa kuiheshimu katiba ya nchi katika utendaji wake na kulisogeza taifa mbele. Mwisho wa siku hakuna atakayempima Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kama amekuwa mama bora au laa, bali atapimwa kwa utendaji wake na jinsi alivyowaongoza Watanzania.

Rais wetu wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Nyerere tulimuita 'Baba wa Taifa,'. Sioni shida kumuita rais wetu wa kwanza mwanamke 'Mama wa Taifa'.