1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Cameron

Abdu Said Mtullya24 Januari 2013

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya Kongamano la uchumi wa dunia, hotuba ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na juu ya mgogoro wa nchini Mali.

https://p.dw.com/p/17R3l
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Reuters

Juu ya Kongamano la uchumi wa dunia linalofanyika katika kitongoji cha burudani,Davos nchini Uswisi,gazeti la"Reutlinger General Anzeiger" linasema soko la dunia linapaswa kuekelekezwa katika lengo sahihi.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa uwezo wa kujenga uchumi utakaohimili misukosuko ndiyo inayopasa kuwa kaulimbiu ya Kongamano hilo.Kwa usemi mwingine lazima pawepo dhamira ya wazi kabisa ya kuleta ustawi,maendeleo na ubunifu katika sekta zote.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema katika hotuba yake aliyoitoa jana kwamba atawapa fursa watu wake kupiga kura ya maoni ili kuchagua iwapo Uingereza iendelee kuwemo katika Umoja wa Ulaya au ijitoe.

Gazeti la"Stuttgarter"linasema,bara la Ulaya linapaswa kutoa jibu la busara kwa Waziri Mkuu wa Uingereza.Lakini kwanza kabisa inapasa kusema,kwamba siasa Cameron ya kuchagua mambo mazuri tu katika Umoja wa Ulaya haikubaliki.Lakini katika upande mwingine litakuwa jambo la busara kuyazingatia malalamiko ya Uingereza juu ya Umoja wa Ulaya.Umoja wa Ulaya unahitaji utaratibu utakaoendeleza mageuzi na kupunguza urasimu.

Mhariri wa gazeti la"Frankfurter Allgemeine" anakubaliana na maoni ya"Stuttgarter" kwamba inapasa kuyasikiliza na kuyazingatia kwa makini anayoyasema Waziri Mkuu Cameron badala ya kumsakama. Hata hivyo gazeti la "Delmenhorster Kreisblatt" linasema hotuba ya Cameron inaonyesha kwamba Waziri mkuu huyo bado ana mawazo ya kizamani.

Gazeti hilo linasema ni jambo la kushangaza kwamba wale wanaofunga breki,ndiyo wale wale wanaolalamika kwamba mambo hayasongi mbele! Hakuna anaepinga mjadala juu ya kuleta mageuzi katika Umoja wa Ulaya.Lakini jinsi Cameron alivyolitoa pendekezo lake,Waziri Mkuu huyo ameenda kinyume na changamoto muhimu za Umoja wa Ulaya.Mawazo ya kitaifa yamepitwa na wakati.


Mgogoro wa Mali bado unaendelea,na ndiyo kusema kwamba majeshi ya Ufaransa yanaendelea kuwamo nchini humo.Na ndiyo sababu,Ufaransa inastahiki kuungwa mkono na nchi zote za magharibi.

Hayo anayasema mhariri wa gazeti la "Die Welt".Anaeleza kuwa magaidi wanajitandaza,kaskazini na magharibi mwa Afrika.Hiyo ni hatari kubwa kwa bara la Ulaya.

Lengo la magaidi ni kulizingira na kulishambulia bara la Ulaya.Wakati Ujerumani na Ufaransa zinaadhimisha mwaka wa 50 wa mkataba wa urafiki baina yao litakuwa shauri zuri kwa Ujerumani na nchi nyingine za magharibi kuziunga mkono hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Ufaransa nchini Mali.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Abdul-Rahman