1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan ataka mchekeshaji aadhibiwe

13 Aprili 2016

Katika tahariri zao, wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya mkasa wa mchekeshaji wa Televisheni ya Ujerumani aliemkashifu Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

https://p.dw.com/p/1IUU3
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/J. Roberts

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amewasilisha malalamiko baada ya kukashifiwa vibaya sana na mchekeshaji wa televisheni ya Ujerumani.

Mchekeshaji huyo Jan Böhmermann alitunga na kulisoma shairi katika makala yake ya televisheni lililosema kuwa Rais Erdogan, anawakandamiza watu wa jamii za wachache, ikiwa pamoja na Wakristo. Pia aliashiria katika shairi hilo kuwa Erdogan anafanya ngono na hayawani.

Rais huyo anataka mchekeshaji wa Ujerumani afunguliwe mashtaka kwa kumkashifu.

Mhariri wa gazeti la "Allgemeine Zeitung" anasema yumkini mchekeshaji huyo Böhmermann alitaka kuanzisha kampeni kubwa ya kujijengea umaarufu. Mhariri wa gazeti hilo anasema labda Böhmermann anajiona kuwa yuko ngazi moja na jarida maarufu la tashtiti "Charlie Hebdo" la nchini Ufaransa. Lakini bado yuko mbali sana na kiwango hicho.

Mhariri wa "Allgemeine Zeitung" anaeleza kuwa mchekeshaji Böhmermann hakuingia vitani kutetea uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa sanaa bali ameomba kutoa mbeu! Wakati huo huo gazeti hilo linatilia maanani katika maoni yake kwamba Rais wa Uturuki anahisi kuwa amevunjiwa hadhi yake ya kibinadamu.

Linalopasa kusema hapa ni kwamba hata watu wanaokiuka haki za binadamu wengine, pia wana hadhi ya ubinadamu.

Gazeti la "Braunschweiger" linakubaliana na mtazamo huo kwa kusema kwamba Erdogan pia anaweza kudai haki nchini Ujerumani. Na hilo hasa ndilo analolifanya. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anasema mahakama sahihi haijui mchezo wa kusalimu amri mbele ya watu wenye mamlaka.

Uhuru wa kutoa maoni unapewa heshima ya juu sana. Na kwa hivyo ni vigumu kufikiria kwamba mchekeshaji Böhmermann ataadhibiwa. Lakini mhariri wa gazeti la "Braunschweiger " anasema hakuna atakaedhurika ikiwa vyombo vya habari vitajiwekea mipaka katika kuutumia uhuru wa kutoa maoni.

Si mara ya kwanza kwa Böhmermann kutifua tufani

Gazeti la "Mittelbayerische" linakumbusha kwamba hii si mara ya kwanza kwa Böhmermann kutifua tufani! Yeye ndiye aliechakachua picha iliyomwonyesha waziri wa fedha wa Ugiriki wa zamani, G. Varoufakis akionyesha kidole cha kebehi!

Mchekeshaji wa Ujerumani Jan Böhmermann
Mchekeshaji wa Ujerumani Jan BöhmermannPicha: picture-alliance/dpa/H. Kaiser

Safari hii mchekeshaji huyo anaweza kuingia katika balaa kubwa zaidi ikiwa serikali ya Ujerumani itasalimu amri mbele ya shinikizo la Uturuki.

Mhariri wa gazeti la "Mittelbayerische" anasema siyo lazima mambo yafike mbali kiasi hicho. Lakini hadhi ya Kansela wa Ujerumani, uhuru wa bwana Böhmermann na hadhi ya taifa la Ujerumani inaweza kuvunjika.

Gazeti la "Rheinpfalz" linatoa maoni juu ya linachoita tamthilia ya nchini Ukraine. Mhariri wa gazeti hilo anasema kile kilichoundwa kutokana na maandamano ya Maidan kinazidi kutumbukia katika mvutano wa kupigania mamlaka.

Mhariri huyo anaeleza kuwa Rais Poroshenko na viongozi wengine wa Ukraine hawajali juu ya washirika wao wa kimataifa. Lakini mhariri huyo anaikumbusha Ukraine kwamba bila ya msaada wa nchi za Magharibi, isingeliweza kusimama yenyewe, kiuchumi na kisiasa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Gazeti la "Rheinpfalz" linawatahadharisha viongozi wa Ukraine juu ya hatari ya nchi yao kusambaratika ikiwa hawataachana na uroho wa mamlaka.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Grace Patricia Kabogo